Hakuna namna unaweza kutenganisha jina la Getrude Mongella na harakati za kijinsia, kwa sababu yeye ni mmoja wa wanawake waliopigania haki za kijinsia kwa ufanisi mkubwa.
Harakati hizi zilipamba moto nchini hasa mwaka 1995, baada ya mama huyu kuteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa Katibu wa Mkutano wa Beijing wa wanawake. Hii ilikuwa ni hatua muhimu katika kudai haki za wanawake kimataifa.
Katika jitihada zao za kutetea haki, wanawake hawa walikumbana na dhihaka, wakituhumiwa kuwa wengi wao ni wanawake walioshindwa kwenye ndoa na hawana uwezo wa kuishi na wanaume.
Hata hivyo, maneno hayo hayakuwa na uzito kwa mwanaharakati na mwanasiasa huyu, ambaye hadi sasa ndoa yake na Silvin Mongella imedumu kwa miaka 56.
Wawili hawa walikutana miaka 58 iliyopita, Getrude akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Silvin akiwa mtumishi wa umma, akihudumu kama Mkurugenzi wa Nyaraka za Taifa.
Kukutana kwao kulianzisha urafiki uliojenga misingi ya uchumba ambao ulizaa ndoa inayodumu hadi leo. Getrude anasema siri ya kudumu kwa ndoa yake, licha ya shughuli za uanaharakati alizojihusisha nazo, ni mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa mume wake.
Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu hivi karibuni, mama huyu anasema aliweza kumtii, kumheshimu, na kumpa nafasi aliyostahili mumewe mara zote.
Mongella anasema alizingatia heshima na utii muda wote bila kujali tofauti ya hali ya kifedha au cheo alichokuwa amemzidi. Anasema hata akiwa na shughuli za uanaharakati, alijitahidi kuwa mke na mama, akitimiza majukumu ya kifamilia kwa ufanisi.
“Kwa kifupi mimi nilimpenda mume wangu na yeye alinipenda kutoka moyoni, ndiyo maana mpaka leo tupo hapa. Kingine ni malezi niliyopata kutoka kwa wazazi wangu; sikuwahi hata siku moja kumsikia baba akimpiga au kumfokea mama, wala mama kumjibu vibaya baba.
“Kwangu hiki ni kitu kikubwa nilichoshuhudia, wazazi wangu walipendana sana hadi uzee wao, nami niliapa nitapendana na mume wangu kama ilivyokuwa kwa wazazi wetu,” anasimulia mama huyo.
Alivyosimama kwenye familia
Getrude anasema wengi walifikiri baada ya kuongoza harakati za kupigania usawa wa kijinsia huenda mambo yangeharibika nyumbani kwake, lakini haikuwa hivyo, walishirikiana kikamilifu na mumewe kwa lengo la kuhakikisha hakuna kinachokwenda kombo ndani ya familia.
“Nilifanya kila linalowezekana ili nibaki kwenye nafasi yangu kama mke na mama wa familia, licha ya kuwa tayari nilishaanza kuaminiwa kwenye nafasi kubwa za uongozi.
“Kila nilipobanwa na majukumu ya kazi, mume wangu alisimama imara kuangalia familia, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto hawapati madhila ya kumkosa mama yao.
Anasema hilo liliwezekana kutokana na kila mmoja kuamini jukumu la kulea watoto ni la kwao wote, hivyo mmoja asipokuwepo mwingine anaziba pengo na watoto wakawa wanajisikia wapo na baba licha ya mama kutokuwepo.
“Inasikitisha kwa sasa zipo jamii nyingi zinamuachia mama malezi ya watoto. Mume wangu hakuwa hivyo, aliona watoto ni wa kwake pamoja na mimi, kwa hiyo tuliwalea pamoja,” anasema mama huyu wa watoto watatu, akiwamo John Mongella, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara.
Maneno hayo ya Getrude yanathibitishwa na mumewe, ambaye anasema miongoni mwa vitu vilivyomfanya kumuunga mkono mkewe katika harakati zake ni heshima aliyokuwa anaipata kutoka kwake.
Anasema pamoja na mke wake kuifanya kazi ya uanaharakati, hajawahi kumkosea heshima na kila akirudi nyumbani kutoka kwenye shughuli yake hiyo akiingia ndani anakuwa mke wa mtu na siyo mwanaharakati aliyekuwa akionekana kwenye majukwaa.
“Hakuacha kutekeleza majukumu yake kama mke na mama wa familia, sikuwa na sababu ya kumuwekea vikwazo, ndiyo maana ninawasihi wanaume wasisite kuunga mkono juhudi ambazo wanawake wao wanazifanya ilimradi tu, haziwavunjii heshima. Tusiache kuwatia moyo na kuchangia wafanye vizuri na kuacha alama kwa jamii,” anasema Mongella.
Kwa nini ndoa za sasa hazidumu
Getrude anasema ndoa za zamani zilikuwa zinadumu kwa kuwa kuolewa ilikuwa ni tendo la heshima, lakini siku hizi wengi wanaingia kwenye taasisi hiyo kwa kufuata mkumbo.
Sababu nyingine ni kupuuzwa kwa michakato ya namna ya kuwapata wachumba na wanandoa kwa kufuata mila na desturi, jambo ambalo lilikuwa linasaidia sana watu kuishi kwenye ndoa zao.
“Zamani suala la mtu kuoa au kuolewa lilikuwa likishirikisha watu wengi na ulikuwa mchakato wa muda mrefu, hadi inapofika wakati mnataka muachane ilikuwa lazima mkifikirie mara mbilimbili mnaenda kuwaambia nini watu.
“Lakini siku hizi watu siku mbili wameokotana huko, hawajajuana wanakuja wanawaambia wazazi wanataka wafunge ndoa na wengine kujihamishia kabisa kwa wakwe au mume hata kabla hawajafunga ndoa.
Kutokana na hayo, mama huyu ametaka mila na desturi za zamani ambazo zilikuwa zina faida katika taasisi hiyo kurejewa, japo hata kama hazitafanana kila kitu.
Pia anashauri vijana kuacha kudeka, kwa kuwa utakuta jambo dogo tu wamekosana ndani ya nyumba wanaenda kushtaki kwa wazazi, wakati hao wazazi wanaoenda kushitaki kwao nao wana yao ndani ya ndoa zao.
Wanandoa wote hawa kwa pamoja wanasema changamoto zinazokabili taasisi ya familia kwa sasa ni ubinafsi ambao mwishowe ndio unazalisha ugomvi.
“Katika maisha, kugombana ni mzigo mkubwa kuliko watu mkipatana, hivyo mkiamua kuishi kwa kupatana basi maisha yatakuwa rahisi tu. Pia katika ndoa tupende kushirikishana wenza kwa kila tunachokifanya ili kujenga familia iliyo bora.
“Hata mimi katika mihangaiko yangu ya kutafuta maisha kila nilichofanya nilihakikisha namshirikisha mume wangu na yeye alifanya hivyo, lakini siku hizi kuna mambo baba hayajui au mama hayajui na hawa watu wanaishi nyumba moja,” anasema Getrude.
Alivyokuwa bosi wa mume wake
Hapa Getrude pia anasimulia katika kufanya kwake kazi maeneo mbalimbali ya Serikali, kuna siku alijikuta yeye ndiyw bosi katika ofisi ya mume wake.
Hii ilikuwa ni mwaka 1982 – 1988 ambapo akiwa Waziri katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, enzi hizo ikiwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, mume wake alikuwa ni Mkurugenzi wa Idara ya Nyaraka katika ofisi hiyo.
Katika kufanya kazi kwao huko, anasema hata siku moja mume wake hakuwahi kubweteka au kufanya mambo yasiyo kisa tu mke wake ndiye bosi.
Lakini pia yeye hakuwahi kumkosea heshima mume wake kwa kuwa tu ni bosi na katika hili anasema hata ilipofika wakati ana dharura na anahitaji ruhusa alifuata utaratibu kama wanaofanya wafanyakazi wengine wa kawaida.
“Mume wangu wakati tunafanya naye kazi na mimi nikiwa bosi wake, hakuniomba appointment nyumbani na mara nyingi nilikuwa napanda naye gari moja, naanza kumshusha kwanza yeye, lakini haniambii chochote mpaka anapofika ofisini.
“Nampenda sana mume wangu, alikuwa smart kwa kweli, nashukuru kumpata mwanaume wa aina yake, kwani angekuwa mwingine ambaye angetaka kuchanganya kazi na mapenzi asingekuwa anahangaika kufuata taratibu,” anasema Getrude.
Kuhusu kufanya kazi ofisi moja na mkewe, Silvin anasema hakuruhusu uhusiano wake uingilie kwenye kazi, hivyo akiwa kazini Getrude alikuwa bosi wake na aliporejea nyumbani alikuwa mke.
“Ni kweli mke wangu alikuwa na cheo kikubwa ambacho mtu yeyote wa chini yake asingeweza kunigusa hata kama ningefanya ujinga, lakini tuliwekeana misingi ya kuheshimu kazi kwanza na mapenzi ni baadaye tukiwa kwetu,” anasema baba huyo.
Nafasi ya watoto katika mafanikio ya wazazi
Pamoja na kufanya kazi nafasi mbalimbali, kubwa lililompa umaarufu Getrude ni kuwa katibu wa mkutano mkuu wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing, China.
Anaeleza kuwa mtoto wake wa pili aitwaye Patrick ndiye aliyemshawishi kuomba nafasi hiyo ilipotangazwa, ikiwa ni muda mfupi tangu ateuliwe kuwa balozi wa Tanzania nchini India.
Anasema wakati nafasi ya Katibu inatangazwa, ilikuwa ni zamu ya nchi za Afrika, wanawake mbalimbali wanaharakati wa haki za wanawake ndani na nje ya nchi walimuomba aiombe kwa kuamini inamfaa kutokana na kumfuatilia mambo aliyokuwa akiyafanya juu ya wanawake.
“Iliniwia vigumu kukubali hili kwa haraka, siku moja nikiwa kwenye wimbi la mawazo mtoto wangu alinigundua siko sawa, akaniuliza shida nini, nikamwambia suala hilo la kuomba nafasi katibu na namna watu walivyokuwa wananishawishi,” anasema na kuongeza:
“Aliniambia mama si umesoma Biblia, ulisoma kile kipengele cha watu waliokuwa wamegawiwa talanta, nikamwambia nimesoma. Akasema wewe umepewa talanta, ila hujui.
“Watu wanakushawishi kwa sababu wameiona talanta uliyonayo, naomba usicheze na Mungu, katumie talanta zako, nami nikaona yale maneno ni ya kweli ndipo nikaamua kuandika barua, kwa msukumo wa mtoto aliyeniambia juu ya talanta zangu ambazo nyingine nilikuwa sizijui na mwishowe kweli nikachaguliwa kuwa Katibu,” anasema.