Katika kila jambo unalofanya kwa watoto wako, iwe ni kwa maneno au vitendo, elewa kwamba lengo kuu ni kuwafundisha na kuwasaidia kuelewa.
Iwe unawasaidia, unawakanya, unawaelewesha au unafanya jambo jingine lolote, mwishowe wanapaswa kujifunza jambo muhimu.
Ukifanya jambo na mtoto wako na asipate funzo lolote, akatoka akiwa hajapata chochote, iwe amecheka au amenuna, basi kama mzazi umeshindwa kutimiza jukumu lako.
Usitazamie vitu au mambo yasiyo halisia kutoka kwa watoto wako. Mfano unakuta mzazi anahamaki kupita kiasi eti kisa mtoto wake amekosea, au amepigana, au amempiga mwingine, au amevunja kitu, au amefeli.
Ni vema uiweke akilini mwako kwamba kwa sababu mtoto wako ana umri mdogo anaweza kufanya chochote cha kitoto, hata kile usichodhani kwamba angefanya.
Usiweke matazamio makubwa sana kwamba yeye ni wa kufaulu tu, yeye ananidhamu wakati wote, siku akifanya tofauti itakuumiza sana na mrejesho wako kwake hautakuwa mzuri. Watoto watafanya makosa kwa sababu ni watoto.
Tafuta namna au mbinu ambayo mwanao hujifunza kwa urahisi.
Njia inayomfaa mtoto wangu inaweza isimfae mtoto wako. Vitu vinavyomfurahisha mtoto wangu vinaweza visiwe vitu vitakavyomfurahisha mtoto wako. Fahamu mtoto wako anajifunza zaidi kwenye njia gani na uitumie hiyo zaidi.
Kuna njia tofauti za watoto kujifunza na kuelewa, kwa mfano, kwa kuona, kwa kusikia, kwa kugusa au kwa kufanya. Jiulize au chunguza, je, mtoto wako hutumia njia gani zaidi?
Wafikie watoto pale walipo
Mtu mwenye shida hufuatwa alipo, siyo kumwambia mbona umeingia kwenye hiyo shida? Usiwe na hofu, usihamaki kwamba mtoto wangu haelewi, chukua muda mfuate alipokwamia, msaidie kutoka, usimlazimishe aweze au afikiri au afanye kama wewe kwa sababu wewe pia ulikosea ulipokuwa unakua.
Wazazi wengi huwalazimisha watoto wao wadogo wafanye kama wao, utasikia; “mimi nilipokuwa na umri kama wewe nilifanya hivi au nilifanya vile,” sasa si wewe?
Muda unatofautiana, mazingira yanatofautiana, malezi pia yanatofautiana. Mwache mtoto wako akue kwa utaratibu wake kama mtoto. Heshimu hatua zake za ukuaji, na anapokutana na changamoto au kuhitaji msaada, jishushe hadi katika ngazi yake ya uelewa.
Zungumza na sehemu ya ubongo wake ambayo unatamani ikusikilize. Kiwango cha juu kabisa cha watoto kufikiri hutokea kwenye eneo la mbele la ubongo wao, sehemu hii inaitwa “front cortex”, lakini sehemu yenye kuongeza woga iko pembeni kwenye kichwa.
Kwa hiyo unapogombana na mtoto na kumtisha, ile sehemu ya woga na kuhamaki ndiyo huamshwa. Ukitaka aelewe, muangalie usoni, elekeza matamshi mbele ya kichwa chake ili ile sehemu ya kufikiria kwenye ubongo wake ndiyo iamshwe na kufanya kazi.
Haihitaji kupayuka ili kumfundisha mtoto, badala yake unatengeneza usugu wa kukaripiwa na woga ambao haumsaidii chochote zaidi ya kuendelea kupanda chuki kali baina yenu.
Mpe uwezo wa kuchagua iwe anapenda au hapendi, watoto wana uchaguzi wa kila kitu, wanajua nini wanataka nini hawataki, nini wanapenda na nini hawapendi. Wana uwezo wa kuchagua kukusikiliza au kutokukusikiliza. Yawezekana ameshindwa kuchagua, hiyo haimaanishi kuwa hana chaguzi, ila inabidi afundishwe kuchagua kwa sababu bado ana uamuzi wa kuchagua na ataendelea kuwa nayo.
Pamoja na kufahamu na kuheshimu haki yao ya kuchagua wanachokitaka, ni muhimu kuwapa uelewa wa athari, kufahamu madhara yatokanayo na uchaguzi wao.
Watoto wasio na ujasiri kwa kawaida hawana kanuni na pia hawaoni athari kwenye maisha, watoto wenye ujasiri wa kati huelekezwa kidogo, wana kanuni na wanajua athari za wanachokifanya.
Simamia katika yale yote unayoyasema. Maanisha unachokiongea, wote tunaaminiwa na watoto wetu, kila tunaposema na kutokutenda kile tulichokisema, ile hali ya uaminifu wao kwetu inashuka hadi inaisha kabisa. Habari njema ni kwamba kwa kadiri tunavyojitahidi kuwa na msimamo, na wao huongeza uaminifu kwetu.
Siyo kwamba uwe mkamilifu, hapana, hata mzazi ana mapungufu yake, lakini la muhimu uwe makini kwenye kusimamia maneno yako. Kadiri unavyozidi kuwa na msimamo kwenye maamuzi yako ndivyo unavyozidi kuaminika zaidi.
Kuna tofauti kubwa sana ya kuhamasisha nidhamu kwa kutumia fujo, mapigano na hasira. Watoto wanahitaji kuona nidhamu siyo kufanyiwa fujo. Onesha upendo hata katika kumuadabisha mwanao. Huna haja ya kutengeneza uadui.
Kuwa kioo cha namna ya nidhamu unayoitaka
Watoto hujifunza zaidi kwa waonavyo kuliko wasikiavyo. Ukitaka wawe na nidhamu kwenye maisha basi ioneshe nidhamu hiyo wewe kwanza. Huwezi kuishi kihasarahasara ukategemea nao waishi vizuri.
Unataka awe msafi? Kuwa msafi wewe kwanza, unataka awe mkweli? Kuwa mkweli wewe kwanza. Kumbuka kwamba wewe ni kioo cha kwanza cha mtoto wako, anakuangalia kwa karibu kila siku.