Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Dodoma
CHAMA Cha Mapunduzi(CCM) kimepitisha jina la Stephen Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrhaman Kinana aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai mwaka 2024.
Jina la Wasira ambaye mwanasiasa mkongwe nchini limetangazwa leo Januari 18 mwaka 2025 jijini Dodoma kupitia Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan sambamba na uwepo wa viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.
Baada ya jina la Wasira kutajwa ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe na nderemo ambapo wajumbe wa mkutano huo walisimama kuashiria kukubali kutangazwa kwa jina lake.
Hivyo baada ya kutagazwa kwa Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti maana yake safu ya juu ya Chama hicho imekamilika na sasa kazi iendelee kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwishoni mwaka huu.
WASIRA NI NANI,AMETOKA WAPI?
Historia ya Stephen Wasira inaonesha alizaliwa mwaka 1945 wilayani Bunda mkoani Mara Mkoa wa Mara na kwa sasa umri wake ni zaidi ya miaka 70.
Kuhusu elimu Wasira alisoma katika shule tatu tofauti, alianza na Shule ya Msingi Bariri 1956-1959, ya pili ni Shule ya Msingi Nyambitilwa 1960–1961 na kisha akamalizia Shule ya Msingi Kisangwa mwaka 1962 – 1963.
Pia Stephen Wasira mwaka 1964–1967, alisoma elimu ya Sekondari katika Chuo cha Ukufunzi Uingereza (British Tutorial College) na kuhitimu kidato cha nne .Hata hivyo akiwa anaendelea na masomo ya sekondari (1965–1967).
Stephen Wasira pia alifanya kazi akiwa msaidizi wa masuala ya maendeleo ya jamii na alipohitimu kidato cha nne alianza kuitumikia Tanu akiwa katibu wa wilaya mwaka 1967-1973.
Mwanasiasa huyo mwenyemisimamo na anayeamini katika uadilifu,uzalendo na kufanya kazi kwa bidii ilipofika mwaka 1975–1982 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mwaka 1982 akateuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington, D.C.
Wakati akiwa huko katika nafasi hiyo pia alikuwa anasoma na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi na Uhusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Amerika (American University) kilichopo Washington DC mwaka 1982–1985.
Wasira alisoma Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Umma kati ya mwaka 1985–1986 na aliporejea nchini kuendelea na utumishi wa uwakilishi wa wananchi, aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 1990-1991.
Pia kati ya mwaka ya 1993–1995 Wasira alisoma tena Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Amerika.
WASIRA NDANI YA CCM
Hata hivyo katika ndani ya Chama Cha Mqpinduzi ,inaonesha kwamba Stephen Wasira
amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kuanzia mwaka 2007 na mwaka 2012 alichaguliwa katika wadhifa huo na tena kwa kura nyingi kuwashinda wajumbe wote wa Tanzania Bara.
Pamoja na hayo pia amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM tangu mwaka 2011 na tena 2013 hadi sasa.
Kwa upande wa ubunge Wasira alianza utumishi wa ubunge akiwa na miaka 25, hii ilikuwa mwaka 1970 aliposhinda ubunge wa Jimbo la Mwibara na akaongoza hadi mwaka 1975 huku Rais Julius Nyerere akimteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Ilipofika mwaka 1985, Stephen Wasira aligombea na kushinda ubunge wa Jimbo la Bunda (wakati huu likiwa limemeguliwa kutoka lilikuwa Jimbo la Mwibara.
Hata hivyo katika kipindi hicho aliteuliwa na Rais Mwinyi kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na baadaye Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo mwaka 1989 hadi 1990.
Wasira kwa wakati ule alikuwa anapambana na Jaji Joseph Warioba (Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu).Hivyo Wasira alishindwa na hali hiyo ilimfanya kuondoka Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na NCCR -Mageuzi wakati huo ikiwika na akachaguliwa kwa kura 18,815 dhidi ya 17,527 za Warioba na hivyo akawa mbunge kupitia NCCR.
Hata hivyo ushindi wa Wasira katika uchaguzi huo Warioba aliamua kukata rufaa Mahakama Kuu nayo ikatengua ubunge wa Wasira mwaka 1996 baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na rafu nyingi.
Pamoja na hayo bado Wasira alikata rufaa kadhaa na hivyo uchaguzi wa marudio ulipofanyika mwaka 1999 Wasira alikuwa amekwishatangaza kuihama NCCR kutokana na siasa za ugomvi na mara hii alimuunga mkono mgombea wa UDP, Victor Kubini lakini mara baada ya uchaguzi huo aliamua kurejea CCM.
Baada ya miaka mitano iliyofuatia (2000 – 2005) na hata minne iliyopita (1996 – 2000), Wasira alijielekeza katika biashara na baadae alirejea katika ulingo wa siasa mwaka 2005 na kushinda kura za maoni ndani ya CCM.
Hivyo Wasira mwaka huo wa 2005 na akapitishwa kugombea ubunge wa Bunda na akapita bila kupingwa.
WASIRA NA NAFASI ZA UWAZIRI
Stephen Wasira chini ya uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete akateuliwa kuwa Waziri wa Maji Januari 2006- Oktoba 2006 wakati ya Novemba 2006 – Novemba 2010 alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Na ilipofika Februari–Mei 2008 pia aliwahi kutumikia kwa muda Ofisi ya Waziri Mkuu akiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, Wasira aligombea ubunge tena Bunda na kushinda kwa asilimia 66.1 na baada ya ushindi huo aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu kabla ya mwaka huu kurudishwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
WASIRA NA URAIS
Kama ambavyo imekuwa kiu ya wanasiasa wengi nchini hasa wanaoamini katika kuwatumikia wananchi Wasira wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 alikuwa ni miongoni mwa wana CCM ambao walihusishwa kuwa na nia ya kugombea nafasi hiyo.