Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya kwanza tangu kianzishwe mwaka 1977 kimepata makamu mwenyekiti Bara mwenye umri mkubwa kuliko waliotangulia.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM ibara ya 114 kifungu kidogo cha (i), CCM ina makamu wenyeviti wawili. Makamu Mwenyekiti Zanzibar ambaye ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na makamu mwenyekiti anayeishi Bara.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM wote hawa wanafanyakazi kwa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, lakini wanaweza kufanya kazi za CCM Tanzania nzima.
Stephen Wasira ambaye mkutano mkuu maalumu wa CCM imemchagua kwa kura nyingi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana ndiye mwenye umri mkubwa.
Wasira mwenye umri wa miaka 80 anakuwa wa kwanza akifuatiwa na Pius Msekwa aliyeshika wadhifa huo kuanzia mwaka 2007-2012 akiwa na umri wa miaka 72.
Wa tatu alikuwa Philip Mangula aliyeshika wadhifa huo kuanzia mwaka 2012-2019 akiwa na miaka 71.
Wengine ni Kinana aliyeshika wadhifa huo kuanzia mwaka 2019-2024 akiwa na miaka 68 na Rashidi Kawawa alishika wadhifa huo akiwa na miaka 64 na John Malecela alishika wadhifa huo akiwa na miaka 58 kuanzia mwaka 1992-2007.
Nafasi ya makamu mwenyekiti Bara ilianza kwa Kawawa mwaka 1990, kabla ya hapo kulikuwa na makamu mwenyekiti mmoja ambaye ni Rais wa SMZ.
CCM iliyozaliwa mwaka 1977, Mwenyekiti wa Taifa alikuwa Mwalimu Nyerere huku makamu wake akiwa Aboud Jumbe wakati huo akiwa na miaka 57.
Nafasi hiyo ilishikwa na Ali Hassan Mwinyi akiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuanzia mwaka 1984-1985 akiwa na miaka 59.
Marais wengine wa Zanzibar waliowahi kushika wadhifa wa makamu mwenyekiti wa CCM ni Idrisa Abdulwakili akiwa na miaka 60, Dk Salmin Amour akiwa na miaka 48, Amani Abeid Karume akiwa na miaka 52, Dk Ali Mohammed Shein alichukua akiwa na miaka 62 na sasa Dk Hussein Mwinyi aliyechukua nafasi hiyo akiwa na umri wa miaka 55.