FC Tanganyika ya DRC Congo iko kwwenye mazungumzo na Beki wa Kitanzania, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ aliyevunja mkataba na FC Lupopo ya nchini humo.
Ninja alijiunga na Lupopo msimu huu akitokea Lubumbashi Sports ya nchini humo ambayo aliichezea kwa msimu mmoja kati ya miwili aliyokuwa amesaini na sababu ya kuachana nayo ni changamoto ya mshahara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ninja alisema anasikiliza ofa ya Tanganyika ambayo imeanza naye mazungumzo.
“Ni kweli naendelea na mazungumzo na Tanganyika lakini hadi sasa bado hatujaelewena baadhi ya vitu,” alisema Ninja.
Kama atasajiliwa kwenye klabu hiyo, Ninja atakuwa amefuata nyayo za George Mpole, Mtanzania mwingine aliyecheza timu tatu tofauti Congo baada ya Lubumbashi, Lupopo na sasa Tanganyika.
Timu hiyo kwenye ligi ya Linafoot iko kundi A na TP Mazembe ikiwa imecheza mechi 11 iko nafasi ya pili na pointi 21 ikishinda michezo saba ikipoteza nne.