Winga mpya Yanga kuanzia hapa

KAMA ulikuwa na hamu kubwa ya kumuona winga mpya wa Yanga, Jonathan Ikangalombo akianza kuitumikia timu hiyo, taarifa njema ni kwamba siku si nyingi utamshuhudia akiliwakilisha chama lake hilo alilojiunga nalo akitokea AS Vita ya kwao DR Congo.

Hiyo ni baada ya Yanga kuishia hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipangia mechi yake ya kiporo kabla ya kuendelea kwa Ligi Kuu Bara.

Kwa mujibu wa Taarifa hiyo ya TFF, winga huyo na beki wa kulia, Israel Mwenda wanatarajiwa kuanza kuitumikia Yanga rasmi katika mechi ya kiporo cha michuano ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa Janauri 25, mwaka huu siku moja kabla ya Simba nayo kula kiporo chake cha michuano hiyo.

Wachezaji hao wawili wamesajiliwa kupitia dirisha dogo la usajili lililofungwa katikati ya wiki hii, huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa na hamu ya kuwaona uwanjani, lakini taarifa ni wataanza na kiporo hicho ya hatua ya 64 Bora.

Ipo hivi. Wakati Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ikitangaza kurejea kwa mechi za Ligi Kuu Bara wiki ya kwanza ya mwezi ujao wa Februari, taarifa mpya ni kwamba Yanga na Simba zitaanza kwanza kula viporo vya mechi za michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kupokezana wikiendi ijayo.

Mechi hizo za hatua ya 64 Bora katika michuano hiyo hazikuchezwa kutokana na timu hizo kubanwa na  ratiba za majukumu ya kimataifa, Simba ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika wakati Yanga ikiwa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi za raundi hiyo zilichezwa Desemba 5-10, 2024 huku zikibaki mbili kukamilisha ili kupata timu 32 kuingia hatua inayofuata kuwania ubingwa wa michuano hiyo unaoshikiliwa na Yanga.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwenda kwa klabu husika, imebainisha mchezo kati ya Yanga na Copco FC ya Mwanza utachezwa Jumamosi ijayo wakati ule wa Simba dhidi ya Kilimanjaro Wonders ukipangwa Jumapili ya Januari 26, 2025.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema: “Tumepokea taarifa ya mchezo wetu dhidi ya Copco umepangwa kufanyika Januari 25, 2025.”

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo, wataikaribisha Copco kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam na kesho yake, Simba nayo itashuka uwanjani hapo kukabiliana na Kilimanjaro Wonders.

Mchezo huo mashabiki wa Yanga wanaweza kupata fursa ya kuliona jembe lao jipya, Jonathan Ikangalombo aliyetambulishwa Januari 15, mwaka huu, siku ambayo dirisha dogo la usajili lilifungwa. Katika kipindi hicho cha usajili, pia Yanga ilimsajili beki Israel Patrick Mwenda kutoka Singida Black Stars.

Ikangalombo ambaye amejiunga na Yanga akitokea AS Vita ya DR Congo, anacheza nafasi ya winga zote mbili kushoto na kulia huku pia akiwa na uwezo wa kucheza eneo la ushambuliaji.

Ikumbukwe katika mechi 30 za 64 Bora ya michuano hiyo timu zilizofuzu ni, Stand United, Biashara United, Mbeya Kwanza, Transit Camp, Town Star, Polisi Tanzania, Songea United, Kiluvya, JKT Tanzania, Leo Tena na Kagera Sugar.

Nyingine ni; Tabora United, Cosmopolitan, Bigman, Giraffe Academy, Geita Gold, Namungo, Coastal Union, Azam, Fountain Gate, Tanzania Prisons, Pamba Jiji, KMC, Mashujaa, Singida Black Stars, Mambali Ushirikiano, Mtibwa Sugar, TMA Stars, Green Warriors na Mbeya City.

Baada ya kuchezwa mechi hizo mbili za viporo, itachezeshwa droo nyingine kupanga ratiba ya hatua ya 32 Bora, ili kusaka timu 16 zitakazoisaka robo fainali. Bingwa mtetezi wa Kombe hilo ni Yanga inayolishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.

Related Posts