Minziro awatega mastaa wapya Pamba

LICHA ya kusajili wachezaji 11 dirisha dogo wakiwemo saba wa kimataifa, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ amesema haitakuwa kazi rahisi kufanya vizuri, lakini itawezekana tu endapo kama wachezaji watatambua majukumu yao na timu kuwa na mshikamano.

Katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu, timu hiyo imewanasa nyota wa kimataifa saba ambao ni washambuliaji, Francois Bakari, Mathew Tegis, Abdulaye Camara na Shassir Nahimana, kipa Mohamed Camara, beki wa kati Modou Camara na winga, Sharrif Ibrahim.

Klabu hiyo pia iliwasajili nyota wazawa, mshambuliaji, Habib Kyombo na viungo washambuliaji, Deus Kaseke, Hamad Majimengi kutoka Singida Black Stars na Zabona Mayombya kutoka Tanzania Prisons.

Timu hiyo inakamata nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 12 baada ya michezo 16, ikishinda miwili, sare sita na kupoteza nane, huku ikifunga mabao saba tu na kuruhusu 16, hivyo, imefanya maboresho makubwa kwenye eneo la ushambuliaji ili kutibu tatizo la umaliziaji na nafasi.

Minziro alisema wanatambua wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanafikia matarajio ya mashabiki wao, hivyo watazitumia wiki mbili zilizobaki kufanya maandalizi mazuri kuiunganisha timu ili ifanye vizuri ligi itakaporejea Februari, mwaka huu.

“Tutajipanga kuhakikisha ndani ya hizi wiki mbili vijana wanarudi katika hali yao ya kawaida, tunafahamu tuna wachezaji wapya ndani ya kikosi siyo kazi rahisi kwa huu muda mfupi lakini tutapambana kwa sababu najua wajibu wa mchezaji ni kutambua majukumu yake hakuna kingine,” alisema Minziro na kuongeza;

“Naamini hizi wiki mbili hata hao maingizo mapya huko walikokuwa hawakuwa wamekaa tu walikuwa wanafanya mazoezi, kwa hiyo wanapojiunga na wenzao kitu kikubwa ni kuelekezana mambo ya mifumo basi naamini kazi itafanyika,” alisema.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake katika mechi 14 za mzunguko wa pili, Minziro alisema; “Tuna kazi ya ziada ya kufanya mbali ya Kocha hata wachezaji wenyewe wanafahamu hilo lazima tuhakikishe tunabaki Ligi Kuu. Kutokana na vijana ambao tumewaongeza na wale waliokuwepo tukiwa na mshikamano naamini kila kitu kitakwenda sawa.”

Related Posts