KOCHA wa Fountain Gate, Mkenya Robert Matano amesema anahitaji zaidi ya wiki mbili ndani ya kikosi hicho ili wachezaji wa timu hiyo waweze kuendana na mifumo yake, licha ya kukiri mapokezi kwa takribani wiki moja yamekuwa mazuri pia kwake.
Matano aliyekuwa anakifundisha kikosi cha Sofapaka ya kwao Kenya, alitangazwa kuiongoza timu hiyo Januari 10, mwaka huu, akichukua nafasi ya Mohamed Muya aliyetimuliwa Desemba 29, mwaka jana baada ya kichapo cha mabao 5-0, dhidi ya Yanga.
“Jambo kubwa hapa ambalo nimekuwa nikipambana nalo kwa takribani wiki moja ni suala la mfumo kwa maana ya kuangalia njia nzuri ya kutengeneza balansi kwa wachezaji nilionao, itanichukua muda kidogo ila kuna maendeleo yanaonekana,” alisema.
Kocha huyo aliongeza wakati Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kurejea kuanzia Februari tayari ameomba viongozi wampatie angalau michezo miwili hadi mitatu ya kirafiki, ambayo itamsaidia ili kuangalia jinsi wachezaji wanavyoyapokea maelekezo yake.
“Nashukuru viongozi wangu wamelifanyia kazi hilo na leo (jana) tulikuwa na mchezo dhidi ya Mbuni FC ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship, lengo ni kuangalia jinsi wachezaji walivyopokea maelekezo mazoezini na kujaribu mifumo tofauti.”
Kocha huyo anayefahamika kwa jina la utani la ‘Special One’, alijiunga na Sofapaka msimu huu baada ya mkataba wake na Tusker FC aliyoingoza kwa miaka sita kuanzia mwaka 2018 kumalizika, huku akitwaa ubingwa wa Kenya msimu wa 2021-2022.
Matano aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za AFC Leopards na Ulinzi Stars, ameiongoza Sofapaka katika jumla ya michezo 15, ya Ligi ya Kenya huku akishinda mitano, sare sita na kupoteza minne akiiacha nafasi ya saba na pointi 21.
Katika kipindi chake cha ukocha kocha huyo, amewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mara nne akifanya hivyo na Sofapaka FC mwaka 2009 ambayo ameshaachana nayo msimu huu na Tusker FC kuanzia msimu wa 2012, 2020-2021, na 2021-2022.