Sabilo, Ludovick waongeza mzuka TMA

BAADA ya TMA kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa nyota wa JKT Tanzania, Sixtus Sabilo na kiungo Venance Ludovick, katibu mkuu wa timu hiyo, Christopher Marcus amesema wachezaji hao watakuwa na msaada mkubwa kwao ndani ya kikosi hicho.

Sabilo aliyewahi kutamba na timu mbalimbali zikiwemo Mbeya City huku kwa upande wa Ludovick aliyetokea Stand United na kuzichezea Mwadui, Kagera Sugar na Geita Gold, wamejiunga na kikosi hicho katika dirisha hili dogo ili kuongezea nguvu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa TMA, Christopher Marcus alisema ushindani wa kupata saini za nyota hao ulikuwa ni mkubwa, ingawa walipambana kwa lengo la kuhakikisha kikosi hicho cha Arusha kinatimiza malengo ya kucheza Ligi Kuu.

“Haikuwa rahisi lakini nashukuru tulipambana na kupata saini zao, moja ya mikakati yetu katika mzunguko huu wa pili ni kuona tunaleta ushindani mkubwa kwa washindani zetu, tunahitaji nafasi za juu tofauti na hapa tulipo kwa sasa,” alisema.

Nyota wengine waliosajiliwa ni kipa, Ismail Saleh Nakapi aliyewahi kutamba na JKT Tanzania kisha kutimkia Stand United, beki wa kati, Wema Sadoki kutokea Tanzania Prisons na kiungo, Asanga Stalon aliyekuwa anakichezea kikosi cha KenGold.

Related Posts