Wakurugenzi Lindi wapewa kazi zao la korosho

Lindi. Wakurugenzi wa halmashauri mkoani hapa wametakiwa kuwasimamia vijana waliopata mafunzo ambayo yametolewa na Bodi ya korosho Tanzania (CBT) kupitia programu ya” Jenga kesho iliyo bora (BBT).

Vijana hao walipewa mafunzo ili wakawasaidie wakulima kuongeza uzalishaji katika zao la korosho kwa kutumia njia za kitaalamu.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku tano jana Jumamosi Januari 18, 2025,  Mkuu wa Wilaya ya Lindi ,Victoria Mwanziva aliyezungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, amewataka wakurugenzi wote kuwasimamia maofisa kilimo hao ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya kuzalisha tani laki sita ifikapo 2026

Mwanziva amesema kuwa vijana hao wameajiriwa na bodi ya korosho kupitia mradi wake wa BBT, hivyo wakurugenzi wanatakiwa kuwapa ushirikiano na kuwasimamia vijana.

“Niwaombe sana wakurugenzi wote kuhakikisha kuwa vijana hawa wanapewa ushirikiano huko kwenye maeneo yenu ili kuleta tija kwenye zao la korosho,” amesema Mwanziva.

Hata hivyo, Mwanziva amewaasa vijana kuhakikisha kuwa wanaishi kulingana na tamaduni za wenyeji wao ili kupata ushirikiano zaidi.

“Mnakwenda maeneo ambayo watu tayari wana utamaduni wao, wakikukaribisha kula mle msikatae, wanavyoishi wao na nyie mnatakiwa kuishi vivyo hivyo, msiende kuleta ‘ustaa’ hamtaweza kufikia malengo mnayoyataka,” amesema pia.

Katika hafla hiyo, Ofisa Kilimo mkoa wa Lindi Hadija Bakili amewataka vijana hao kuvaa uhusika na kwenda kuwasaidia wakulima, kwa kutoa ushauri na kufufua mashamba pori ili kuweza kuleta tija kwenye zao la korosho na kufikia malengo.

“Tunaenda kwa wakulima mnatakiwa kuvaa uhusika kama ofisa kilimo kweli na kuwashauri wakulima ulimaji wa tija na kuweza kufufua mashamba pori ambayo hayajaendelezwa,” amesema Bakili

Mmoja wa wanafunzi waliopata mafunzo hayo Saidi Bakari amewahakikishia viongozi pamoja na bodi ya korosho , kuwa wanakwenda kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

“Niwahakikishie kuwa hatutawaangusha viongozi wetu pamoja na bodi ya korosho kwani mmetuamini na sisi tutakwenda kufanya kazi ili kufikia malengo,” amesema Bakari.

Kaimu Mkurugenzi wa bodi ya korosho Tanzania (CBT) Magire Maregesi amesema kuwa kupitia mafunzo waliyopewa wao kama bodi, hawatarajii mwakani kuona  korosho chafu na mbovu.

“Sisi kama bodi ya korosho hatutategemea kuona korosho chafu na mbovu, ifikapo mwakani nyie mtakwenda kuondoa korosho chafu na mbovu ili  kufikia malengo yetu,” amesema Maregesi.

Katika programu hiyo vijana 150 wamepewa mafunzo ya kwenda kusimamia viuatilifu kwa wakulima, kwenda kufufua mashamba pori pamoja na kwenda kusimamia ubora wa korosho.

Related Posts