Madenge aja kivingine Biashara United

KOCHA wa Biashara United, Omary Madenge amesema kwa sasa kikosi hicho kinapigania kubaki katika Ligi ya Championship kwa msimu ujao, baada ya malengo yao ya kukipandisha Ligi Kuu Bara kukwama kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza.

Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya timu hiyo kupokwa pointi 15, kutokana na kuandamwa na ukata ulioifanya kushindwa kusafiri kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya kucheza mchezo wake na Mbeya City uliotakiwa kuchezwa Desemba 3, mwaka jana.

“Kwa sasa malengo yetu ni kubaki katika Ligi ya Championship msimu ujao, ni ngumu kusogea juu zaidi kutokana na gepu la pointi lililopo kwa wapinzani wetu, suala la kuibakisha inawezekana na ndicho kipaumbele cha kwanza mzunguko wa pili.”

Madenge aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi ndani ya kikosi hicho kabla ya kuanza kukifundisha baada ya kuondoka kwa Mussa Rashid, alisema licha ya changamoto mbalimbali ila wadau na mashabiki wa soka wa Mara waendelee kuiunga mkono timu hiyo.

Kitendo cha kupokwa pointi 15, kimeifanya timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2021-2022, kuendelea kunyong’onyea, kwani licha ya kushinda michezo minne, sare minne na kupoteza saba, ila kinaburuza mkiani baada ya kubakiwa na pointi moja tu.

Related Posts