YANGA Princess dirisha hili dogo limesajili washambuliaji wawili wa kimataifa, hata hivyo, wanakabiliwa na changamoto ya vibali (ITC).
Wachezaji hao ni Mukandayisenga Jeannine kutokea Rayon Sports ya Rwanda na Juliet Nalukenge wa Uganda.
Kiongozi mmoja wa Yanga (hakutaka jina lake litajwe) alisema hadi sasa hawajatambulisha wachezaji hao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo vibali.
Aliongeza, Jeannine hajakamilisha ITC yake na taratibu nyingine za kimakubaliano na klabu yake ya Rayon ambayo bado alikuwa na mkataba wa miezi sita.
“Yupo na timu na anafanya nayo mazoezi, kuna vitu havijakamilika ndiyo maana hajatambulishwa lakini naamini hadi ligi itakapoanza mambo yatakuwa fresh,” alisema kiongozi huyo.
Kuhusu Nalukenge alisema “Tulishindwa kuelewena kwenye baadhi ya vitu alikuwa tayari yupo nchini na alianza mazoezi na timu lakini kaondoka ghafla.”
Hadi sasa Yanga imetambulisha wachezaji watatu wa ndani, kipa Zubeda Mgunda, kiungo Protasia Mbunda na Diana Mnally.