Odero: Nimetumwa na mbingu kugombea uenyekiti Chadema

Dar es Salaam. Katika nyakati za lala salama kuelekea uchaguzi mkuu wa Chadema, mgombea uenyekiti Odero Charles Odero amesisitiza kuwa, hakugombea kwa bahati mbaya, bali anatekeleza maelekezo ya Roho Mtakatifu na mbinguni.

Mpaka sasa kuna wagombea watatu wa uenyekiti Chadema katika uchaguzi utakaofanyika Jumanne Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam, akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe na makamu wake Tundu Lissu wanaopeana ushindani mkali.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi leo Januari 19, 2025 jijini Dar es Salaam, Odero amesema haogopi ushindani wa Mbowe na Lissu.

“Mimi sijawasiliana na Roho Mtakatifu kuhusu kujitoa,” amesema Odero alipoulizwa kama ana mpango wa kujitoa dakika za mwisho.

Ameongeza: “Sikugombea kwa bahati mbaya, nimegombea kwa kufanya mawasiliano na mbingu na nimejiridhisha, kwa hiyo sina mpango wowote kwamba ninaweza kujitoa.

“Ukisema nitamchagua nani kati ya wagombea watatu, chaguo la kwanza ni Odero, chaguo la pili ni Odero na chaguo la tatu ni Odero.”

Amesisitiza kuwa Mungu ndio amemweka kugombea nafasi hiyo.

“Bahati nzuri Mungu ameniweka, na kwenye orodha niko katikati na hii sio mbaya, wameniweka katikati kwa makusudi ya Mungu, kwamba pembeni kwangu kuna Lissu na kushoto kwangu kuna Freeman Mbowe,” amesema.

Mbali na Mungu, Odero amesema ana mtaji wa wapiga kura anaowasiliana nao.

“Mimi ninafanya mawasiliano na wapiga kura, sipambani na umaarufu, kwenye siasa hatuhitaji umaarufu, tunahitaji mtu sahihi kwa wakati sahihi, mtu ambaye anaweza kuunganisha chama chetu kikawa sawa. Mtu anayeweza kwenda kwenye mapambano ya kura ya chama chetu ni mimi,” amesema.

Ametaja maeneo anayoungwa mkono kuwa pamoja na Pemba, Karagwe, Tunduma, Rombo (Kilimanjaro), Kigoma Kigamboni (Dar es Salaam), Mtwara na Mpwapwa (Dodoma).

“Watu wamevutiwa na kauli yangu kwamba mbele kuna mwanga, hapo mbele tunakwenda kushinda ubunge, tunakwenda kushinda urais, tunakwenda kuwa na chama bora.”

Amesema hatumii uchaguzi huo kujitangaza, kwani yeye ni mtu makini na sahihi kwa ajili ya kuleta mageuzi ya kisiasa katika chama hiki kwa ajili ya kutwaa Dola.

“Ninaogombea nao kaka zangu wawili (Mbowe na Lissu), wamekuwepo kwa miaka kadhaa na mimi nimekuwepo sio kwenye ngazi za uamuzi, lakini sasa ni wakati sahihi kuwa kiongozi.

“Kaka zangu tunawezana na tunatoshana. Kwa Waluo kuna msemo, Mundu kwa mundu yaani mtu kwa mtu, kwa hiyo tunapishana kwa mbinu na mikakati.

Miongoni mwa mambo anayojivunia Odero ni kupigania haki za Watanzania ikiwa pamoja na kupinga tozo za miamala ya simu zilizoanzishwa na Serikali mwaka 2022.

“Leo Watanzania wanafurahia tozo ya miamala ya simu kwa sababu huyu raia aliona kwamba tozo hizo zilianzishwa kinyume cha sheria.

“Japo kesi ile hatukushinda, lakini iliifungua macho Serikali na kuona kuwa raia kumbe wamekasirika, kwa hiyo baadaye mmeona wamepunguza,” amesema.

Odero ametaja pia  kesi aliyofungua dhidi ya Ofisi ya Taifa ya Mashitaka katika Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Salaam, akipinga watu kufunguliwa mashitaka kabla upelelezi haujakamilika.

“Japo kuwa hatukushinda kesi hiyo moja kwa moja, lakini kesi hiyo ilisababisha kuwekwa mkazo kwamba kabla ya kumkamata mtu ni lazima ufanye upelelezi wa kutosha.

“Kwa sababu kilikuwa ni kitendo cha kunyima na kutweza uhuru wa mtu, halafu ukifika mahakamani unasema upelelezi bado,” amesema.

Kazi nyingine anazojivunia ni utetezi wa haki za raia wa nchi hii na hasa jamii ya wafugaji katika ardhi kwa watu wa Loliondo, Ngorongoro (Arusha) na Nyatwali Bunda (Mara), Mkoa wa Morogoro, Msomera (Tanga) na maeneo mengine.

Odero anasema miongoni mwa malengo yake ni kuwawezesha Watanzania kupata mahitaji manne muhimu ambayo ni uwezo wa chakula bora, uwezo wa mavazi bora, uwezo wa makazi na uwezo wa kuwasiliana.

“Kwanza ni kusimamia makusudi au madhumuni ya chama kushika dola. Kazi yangu mimi kama mwenyekiti ni kama kocha, kuandaa timu kwenda kucheza na kushinda uwanjani pale tupate kombe, kwa kuuongoza halmashauri, kuongoza bunge na nchi kwa maana ya rais,” amesema.

Pia amesema ana malengo ya kufanya mageuzi ndani ya chama hicho ili kiendane na wakati.

Miongoni mwa mageuzi hayo ni kuanzishwa kwa bodi huru ya uchaguzi na mahakama maalum ya kushughulikia mashitaka ndani ya chama.

“Natamani uchaguzi wetu wa ndani uratibiwe na bodi huru ya uchaguzi, natamamni vilevile kuwe na mahakama ya kichama inayosikiliza na kuamua na kutoa haki pindi malalamiko yakitokea,” amesema.

Mageuzi mengine anayofikiria ni pamoja na mifumo ya uchaguzi na nafasi za juu.

“Je, tunahitaji ya kukusanyika Mlimani City au Dodoma kwa ajili ya uchaguzi wa mwenyekiti? Je, hatuwezi kufikiria kwamba wakati umefika wanachama nao wawe sehemu ya chama hiki waweze kumchagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti?

“Je, tuwe na makamu mwenyekiti ambaye anasubiri kama mwenyekiti hayupo ndio anashika madaraka? Je, tuwe na wajumbe wa kamati kuu ambao hawana majukumu mahsusi?

Kuhusu kamati kuu, amesema anatarajia kuwa na wajumbe wasiozidi 15 na watakuwa kila mmoja atapangiwa majukumu kulingana na ujuzi wake.

“Kwa hiyo tunaweza kusema wewe utakuwa mjumbe wa kamati kuu unayeshughulikia elimu, kwa hiyo tukikutana kwenye kamati kuu unaleta taarifa ya elimu.

“Tunakuwa na mjumbe anayeshughulikia mambo ya nje, mambo ya ndani anayeshughulikia masuala ya habari, viongozi wa dini, jumuiya za wafanyabiashara na mengineyo,” amesema.  

Lengo lake lingine ni kuboresha uchumi wa chama na wanachama.

Amesema atatekeleza hilo kwa kuleta hamasa kwa wanachama kukichangia chama.

“Mathalani tukiwa ana wanachama nchi nzima na kila mwaka akatoa Sh2, 500 maana yake unazungumzia Sh2.5 bilioni. Ukigawa Sh2, 500 kwa miezi 12 utaona kila mwanachama atalipa Sh208 kwa mwezi. Hapo ni wanachama tu, bado mbinu nyingine kama harambee, marafiki zetu.

“Hizo Sh2.5 bilioni tunaweza kutumia kwenye operesheni za chama. Hiyo ni mwanzo tu, tunahitakji kuwekeza kwenye ardhi, tunahitaji kuwekeza kwenye majengo, kujenga ofisi kwenye wilaya mbalimbali,” amesema.  

Odero mwenye shahada ya kwanza ya mawasiliano ya umma Kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), ni kada wa Chadema kutoka jimbo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha tangu mwaka 2000.

Amewahi kuwa mwenyekiti wa tawi, mwenyekiti wa kata, mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) Mkoa wa Arusha, mjumbe wa Mkutano mkuu wa Taifa, mjumbe wa Baraza kuu Taifa na mwenyekiti wa wilaya.

Pia amewahi kushiriki kama mtaalamu wa mafunzo ya Chadema, mkufunzi wa masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika Kanda ya Kaskazini.

Aliwahi kugombea udiwani Kata ya Baraa jijini Arusha lakini hakufanikiwa.

Related Posts