Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeimarisha uchumi kupitia uwekezaji katika nishati, maji, afya, elimu, na usafirishaji hivyo kiwango halisi cha ukuaji wa Pato la Taifa kimeongezeka kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi asilimia 5.1 mwaka 2023.
Aidha, amesema Serikali imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 3 mwaka 2024 kutoka asilimia 3.1 mwaka 2020.
Ameyasema hayo wakati akiwasilisha utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya uchaguzi wa mwaka Novemba 2020 hadi Desemba 2024 upande wa Tanzania bara katika siku ya pili ya Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, leo Januari 19, 2025.
“Mapato ya ndani yaliongezeka kufikia Sh13.54 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh8.1 trilioni mwaka 2020. Idadi ya walipa kodi iliongezeka hadi milioni 6.4, na Serikali imeondoa kodi zisizo na tija ili kuchochea maendeleo,” amesema.
Akizungumzia upande wa sekta ya fedha amesema mafanikio yaliyopatikana ni kuongezeka kwa wastani wa mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka sh1.47 trilioni Novemba, 2020 hadi Sh2.37 trilioni Novemba, 2024.
“Madeni yaliyohakikiwa ya Sh3.47 trilioni yamelipwa kwa makandarasi, watumishi, watoa huduma, wazabuni na madeni mengineyo ya kimkataba. Mikopo ya Sh693.9 bilioni ilitolewa na Serikali kwa wanufaika zaidi ya milioni 1.7 katika sekta za kilimo, mifugo, na uvuvi,” amebainisha.
Katika sekta ya kilimo Serikali imeimarisha Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ambapo vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka 2,150 mwaka 2020 hadi 4,060 mwaka 2024. Mazao yaliyouzwa ni pamoja na choroko, dengu, mpunga, mbaazi, kahawa, korosho na pamba.
“Kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 18.6 mwaka 2020 hadi tani milioni 22.8 mwaka 2024. Uzalishaji huo ulichagizwa na kuongezeka kwa upatikanaji wa mbolea kwa asilimia 107 kutoka tani 586,604 mwaka 2020 hadi tani 1,213,729 mwaka 2024,” amesema.
Katika kupambana na umasikini na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi amesema Serikali imefanikiwa kutoa huduma za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kaya za walengwa 1,357,965 katika vijiji, mitaa na shehia 17,260 Tanzania Bara na Zanzibar;
Upande wa sekta ya mifugo katika kipindi cha miaka minne Serikali imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita bilioni 3.1 mwaka 2020 hadi lita bilioni 3.97 mwaka 2024 kulikochagizwa na ongezeko la ng’ombe wa maziwa kutoka milioni 1.2 hadi milioni 1.4 mwaka 2024.
“Viwanda vya kuchakata nyama vimeongezeka kutoka vitatu hadi saba, na kuchangia kuongezeka kwa nyama inayouzwa nje kutoka tani 1,669 hadi tani 14,701. Aidha kuwapa mafunzo kwa vijana 240 katika vituo nane vilivyoanzishwa kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT),”
Serikali imeimarisha miundombinu ya usafiri kwa kutekeleza miradi mikubwa ya reli, anga na bandari.
“Kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar es Salaam hadi Makutupora (km. 722) ambapo huduma ya kusafirisha abiria kati ya Dar es Saalam – Morogoro – Dodoma zilianza kutolewa rasmi mwishoni mwa mwezi Juni, 2024.
“Tangu kuzinduliwa kwa huduma ya usafiri kwa kutumia treni ya SGR, Agosti 2024 hadi Desemba 11, 2024, zaidi ya abiria milioni 1.2 wamesafiri kwa kutumia treni hiyo na hivyo kupunguza muda wa kusafiri, kuongeza tija katika biashara na uchumi kwa ujumla na kuingiza jumla ya Sh30 bilioni,” amebainisha.
Amesema Serikali pia imeongeza idadi ya ndege za abiria na ndege za mizigo na ATCL sasa inamiliki ndege 16.
Serikali imeandaa mipango na mikakati ya kupambana na majanga, ikiwa ni pamoja na kuandaa Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa (2022) na Mkakati wa Afya Moja.
Aidha kuimarisha maghala ya huduma za kibinadamu na kujenga Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa Dodoma.