Baadhi ya wanachama Dodoma watangaza kumuunga mkono Lissu

Dodoma. Ikiwa imebaki siku moja kuelekea kwenye mkutano mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo pia kutakuwa na uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho, baadhi ya wanachama mkoani Dodoma wametangaza kumuunga mkono Tundu Lissu.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo jumapili Januari 19, 2025 jijini Dodoma wanachama hao wamesema kuwa wanachohitaji kwa sasa ni mabadiliko chanya ndani ya chama hicho, ambayo wamekuwa wakiyasubiri kwa muda mrefu bila mafanikio

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Dodoma, Steven Karashani amesema wanaheshimu mchango mkubwa uliofanywa na Freeman Mbowe kukijenga na kukiimarisha chama hicho, lakini ni wakati sasa wa yeye kupumzika kwa heshima na kumwachia Lissu aongoze chama hicho.

Amesema kwa sasa chama kinahitaji mabadiliko makubwa ambayo Mbowe hajayafanya kwa kipindi kirefu na wanaamini Lissu akiingia madarakani, ataleta mabadiliko hayo ambayo wananchi na wanachama wa Chadema wameyasubiri kwa muda mrefu.

“Hapa tunapoongea tuwawakilisha wanachama kutoka kwenye majimbo yote 10 ya mkoa wa Dodoma, wametutuma tukamchague Tundu Lissu ndio awe mwenyekiti wetu wa Taifa,” amesema Karashani.

Kwa upande wake,  Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Godfrey Kimario amesema wajumbe wote wa mkutano mkuu wa Chadema Mkoa wa Dodoma wamekubaliana kupeleka kura zote kwa Lissu ili aweze kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho.

Amesema endapo Mbowe atashinda kwenye uchaguzi huo na kuendelea na nafasi ya mwenyekiti Taifa, wao kama wanachama watachukua maamuzi magumu ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kauli yoyote itakayotolewa na Lissu.

“Endapo Mbowe atashinda uchaguzi huu basi sisi tutachukua maamuzi magumu ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kauli yoyote itakayotolewa na Tundu Lissu baada ya uchaguzi, lakini ni wakati wa Mbowe kuondoka,” amesema Kimario.

Naye Mjumbe wa Baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha) kutoka Kata ya Kikuyu Kaskazini, Rukia Said amesema wanamuunga mkono Tundu Lissu kwa sababu mwenyekiti wa sasa ameshindwa kukiletea chama mabadiliko wanayoyahitaji ikiwa ni pamoja na kutetea haki za wanachama waliopokonywa haki zao wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa tulionewa na kudhulumiwa haki zetu lakini mwenyekiti hakutoa tamko lolote la kuonyesha kuwa tumedhulumiwa haki yetu sana sana tunamwona kwenye mabango akiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano mkuu wa CCM, huyu hatufai,” amesema Rukia.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na makatibu wa Chadema wilaya zote za mkoa wa Dodoma, wenyeviti na wajumbe wa kamati tendaji ya mkoa.

Related Posts