Mwanza. Askofu Oscar Lema wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amewekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria.
Ibada ya kumuweka wakfu askofu huyo imefanyika leo Jumapili Januari 19,2025, katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Imani Kanisa Kuu lililopo Mtaa wa Mission Mwanza na kuhudhuriwa na mamia ya waumini wa viongozi wa kanisa hilo.
Hafla ya kumuweka wakfu kiongozi huyo wa kiroho imefanyika kwa kuzingatia Sheria namba 11 (1) (a) na Kanuni ya 21 ya Katiba ya Kanisa la KKKT.
Akitoa neno kwa askofu huyo, Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa amemtaka kutojitenga na waumini badala yake awatumikie kwa kujitoa kwa kuwa ndiyo jukumu lake bila kuwagawa waumini hao.
Pia, amemtaka askofu huyo kuepuka tamaa badala yake afanye kazi yake kwa bidii kwa kile alichodai Mungu humlipa mtu anayefanya kazi kwa bidii na siyo mwenye tamaa.
“Maandiko matakatifu yanasema Mungu atawabariki wanaomtii na wanaofanya kazi na siyo wezi. Ikiwa mtu hataki kufanya kazi basi asile, popote duniani hasa unaposimamia uhai,” amesema Dk Malasusa.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi amemuomba Askofu Lema kuhimiza mambo manne wakati wa utumishi wake katika wadhfa huo.
Amesema mambo hayo ni pamoja na kuhimiza umoja na mshikamano, amani na utulivu, kuongoza kwa hekima na uwajibikaji sambamba na kuwa kiunganishi kizuri kati ya waumini wa kanisa hilo na Serikali ili kuleta maendeleo kwa jamii.
“Viongozi wa dini mna wajibu wa kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kulindwa nchini. Amani ni muhimu katika maendeleo ya nchi na Serikali inatambua mchango wenu viongozi wa dini,” amesema profesa Kabudi.
Awali, Askofu Malasusa aliwataka waumini na viongozi wa KKKT kumpokea Askofu Lema na kushirikiana naye kwa kile alichodai jukumu la kuijenga dayosisi hiyo liko mikononi mwake.
“Msifanye kazi wenyewe mtende kazi na Bwana (Mungu) kanyaga ardhi ya Mwanza polepole, usijifutue, tufanye kazi pamoja na Mungu, nyumba zetu zitabarikiwa,” amesema Askofu Malasusa.
Muumini wa Kanisa hilo, Esther Juma amesema anaamini kupitia askofu huyo, waumini wanaenda kuunganishwa na KKKT kumrudia Mungu kwa kutenda kama ambavyo vitabu vitakatifu vinavyoelekeza.
“Askofu Lema tunamfahamu amekuwa na mchango mkubwa hususan ni kutatua changamoto za watu mbalimbali wakiwemo wana ndoa tangu akiwa mchungaji. Kuwekwa wakfu kuwa Askofu tunaamini atahimiza sana umoja na kulijenga kanisa,” amesema Esther.
Mbali na Askofu Lema, ibada hiyo pia imemuweka wakfu, Mchungaji Steven John kuwa Askofu Msaidizi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria.