Saa 48 za lala salama uchaguzi Chadema

Dar es Salaam. Safu ya uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitaifa inatarajiwa kukamilika ndani ya saa 48 kuanzia kesho Jumatatu, Januari 20, 2025 tukio linalotabiriwa kugubikwa na mikikimikiki ya ushindani ndani na nje ya ukumbi.

Ni saa 48 za moto, kutokana na uhalisia wa ushindani unaosababishwa na nguvu na ushawishi walionao wagombea wa nafasi mbalimbali za kukamilisha safu hiyo ya uongozi.

Katika saa 24 za kwanza, kutafanyika mkutano wa Baraza Kuu la Chadema unaoanza kesho Jumatatu na ndio unaobeba hatma ya kina nani watakaokuwa wajumbe wanane wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Saa hizo zitafuatiwa na nyingine 24 za mkutano mkuu wa uchaguzi utakaofanyika Jumanne ya Januari 21, 2025. Ndani ya muda huo, atachaguliwa mwenyekiti taifa, kati ya Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Charles Odero na makamu wake bara na Zanzibar.

Ingawa matukio hayo yamepangwa kufanyika kwa saa 24 kila moja, uzoefu wa mikutano iliyotangulia ya Bazecha (Baraza la Wazee Chadema), Bawacha (Baraza la Wanawake Chadema) na Bavicha (Baraza la Vijana Chadema), unaonyesha huenda vikao hivyo vikachukua zaidi ya saa 48.

Mkutano mkuu wa uchaguzi wa Bavicha uliofanyika Januari 13, ulipaswa kutamatika baada ya saa 24, lakini ulifika saa 1:15 jioni ya Januari 14.

Kwa upande wa Bazecha, walimaliza mkutano asubuhi ya Januari 14, tangu Januari 13 siku waliyoanza mkutano huo wa uchaguzi, huku Bawacha ikichukua siku mbili kuanzia Januari 16 hadi 18, mwaka huu.

Ni saa 48 za moto, kwa sababu kila upande kati ya Lissu na Mbowe, unaamini una nguvu na ushawishi wa kutosheleza imani za wajumbe kuuchagua kukiongoza chama hicho kwa miaka mitano ijayo, kama inavyoelezwa na wanazuoni wa sayansi ya siasa.

“Kambi hizi mbili (Lissu na Mbowe) zimevuta sana hisia za wapiga kura. Kwa hiyo tutarajie yeyote kati yao kuibuka mshindi ingawa kwa tofauti ndogo sana ya kumshinda mwenzake, lakini kwa sasa kila mmoja anajiona ana nafasi sawa,” amesema Dk Revocatus Kabobe.

Mkutano wa baraza kuu unaoanza kesho Jumatatu katika ukumbi Mlimani City, jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine utawachagua wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, ambao ndio wawakilishi wa wanachama katika uamuzi wa mustakabali wa Chadema.

Baraza kuu la chama hicho kikuu cha upinzani linaundwa na viongozi mbalimbali wa Chadema, wakiwemo wajumbe wa kamati kuu, makamu wenyeviti wa kanda, makatibu wa kanda na watunza hazina wa kanda.

Wajumbe wengine wa baraza kuu la chama hicho ni wenyeviti wa baraza la uongozi mkoa, makatibu wa mikoa, wajumbe watano watakaochaguliwa na mkutano mkuu wa kila Baraza (Bavicha, Bawacha na Bazecha) wenyeviti wa wilaya kichama na makatibu wao.

Mkutano mkuu wa Chadema, utafanyika Jumanne katika Ukumbi wa Mlimani City na ndio utakaoondoa ubishi wa kati ya Lissu, Mbowe na Odero nani atakayekuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa.

Mkutano huo kwa Chadema, unaundwa na wajumbe wote wa kamati kuu, wajumbe wa baraza kuu, wenyeviti wa wilaya/majimbo na makatibu wote wa majimbo/wilaya.

Wajumbe wengine wa mkutano huo ni wabunge wa jamhuri ya muungano, wajumbe wa baraza la wawakilishi Zanzibar wanaotokana Chadema, wajumbe 20 watakaochaguliwa na mikutano mikuu ya Bazecha, Bavicha na Bawacha.

Pia, watakaokuwepo ni mjumbe mwakilishi wa kila jimbo au wilaya, viongozi wa kitaifa wa mabaraza, ambao sio wajumbe wa kamati kuu.

Saa 48 za mkutano huo wa uchaguzi wa Chadema, zitakuwa za moto, kutokana na ushindani wa wagombea hasa wa uenyekiti yaani Mbowe na Lissu, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe.

Kwa mujibu wa Dk Kabobe, wagombea hao wana nguvu na ushawishi unaofanana au kukaribiana ndani ya chama hicho, hivyo ushindani wao utazifanya saa za mkutano huo kuwa za moto.

“Wote hawa wanakaribia kuwa na ushawishi sawa ndani ya chama na hilo limejionesha kwenye kampeni zao na mgawanyiko uliopo hasa kwenye chaguzi za mabaraza zilizopita,” ameeleza.

Hata hivyo, ameeleza kwa hali ilivyo hatarajii mshindi apatikane kwa kumzidi mwenzake kura nyingi zaidi kama ilivyozoeleka.

“Utakumbuka tangu Mbowe apate nafasi ya uenyekiti mara zote kwenye chaguzi ameshinda kwa zaidi ya asilimia 95. Zamu hii naona tofauti kubwa kwenye hili,” amesema Dk Kabobe.

Mwanazuoni huyo amekwenda mbali zaidi ni kueleza hadi sasa haoni upande wenye uhakika wa kushinda kulingana na hali halisi ilivyo.

“Kambi hizi mbili zimevuta sana hisia za wapiga kura. Kwa hiyo tutarajie yeyote kati yao kuibuka mshindi ingawa kwa tofauti ndogo sana ya kumshinda mwenzake,” amesema.

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Lusungu Mubofu amesema saa hizo 48 hazitakuwa lelemama, kwa kuwa ndizo zitakazoamua hatma ya chama hicho cha upinzani.

Kwa mujibu wa Mubofu, ndani ya saa hizo atajulikana mwenyekiti atakayeiongoza Chadema kwa miaka mitano na pengine kukawa na mpasuko ndani ya chama hicho kwa yeyote atakayeshinda.

“Kimsingi saa 48 zijazo zinakwenda kueleza hatma ya Chadema na huenda kukawa na mpasuko mkubwa zaidi kwa yoyote atakayeshinda nafasi ya mwenyekiti.

“Tutaona makundi makubwa ndani ya chama, inabaki wao kama chama kutafakari kama makundi yatakoma baada ya uchaguzi au la,” amesema.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameandika ni zaidi ya siku ya mkutano mkuu wa Chadema, kwa kuwa ni kumbukizi ya chama hicho kupata usajili kamili mwaka 1993 baada ya kuasisiwa 1992.

Kwa mujibu wa Mnyika, Januari 21 ni siku ya Chadema inayobebwa na ujumbe wa ‘Stronger Together.’

“Tunapoelekea kuadhimisha siku hii ni rai yangu kuwa leo tuwakumbuke kwa kuwataja kwa majina na kuwaombea wote waliouawa katika mapambano ya kudai haki tangu kuanzishwa kwa Chadema,” ameandika.

Katika chapisho lake hilo, amewataka baadhi ya watu hao ni Ally Kibao, Alfonce Mawazo na Daudi Mwangosi.

“Nitumie nafasi hii kuwatakia pia safari njema wajumbe wote wa baraza kuu wanaopaswa kufika Makao Makuu Mikocheni leo tarehe 19 Januari 2025 kwa ajili ya kujisajili.”

Amesema mkutano wa baraza kuu pia, utafanyika katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, kama ilivyo kwa mkutano mkuu wa leo Jumatatu.

Related Posts