Dk Tulia alia na mila kandamizi, kikwazo kufikia usawa wa kijinsia

Arusha. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, amesema mila na tamaduni kandamizi, ikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji, ukosefu wa umiliki wa ardhi, na nafasi chache za wanawake katika uongozi, bado ni vikwazo vikubwa vya kufikia usawa wa kijinsia.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kuchukua hatua madhubuti ili kubomoa mifumo hiyo iliyojikita kwenye jamii na kuvunja minyororo ya dhuluma inayowakandamiza wanawake na watoto.

Kauli huyi imetolewa leo Jumapili, Januari 19, 2025, Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Shally Raymond, aliyemwakilisha Dk Tulia katika mbio za kuadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) zilizofanyika Arusha.

“Mila kandamizi kama ndoa za utotoni, ukeketaji, umiliki wa ardhi na ukosefu wa nafasi katika maamuzi bado ni changamoto kubwa katika kufikia usawa wa kijinsia. Tunaposherehekea jubilei hii, ni wakati mwafaka wa kutafakari changamoto hizi kwa kina,” amesema Dk Tulia.

Amesema juhudi za kuhamasisha jamii kuhusu haki za kijinsia ni muhimu, hasa ikizingatiwa kuwa mifumo mingi ya kijamii imepitwa na wakati na inazuia maendeleo ya wanawake na watoto.

Spika huyo amesema ushiriki wa wanaume katika mabadiliko ya kijamii ni muhimu katika kubadili mitazamo hasi dhidi ya wanawake.

Majaji wanawake kichocheo cha mabadiliko

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, wanawake majaji na mahakimu wakiwa katika nafasi za uamuzi ni rasilimali muhimu katika kuleta mabadiliko chanya.

“Wanawake hawa wamepata fursa ya kipekee ya elimu na nafasi za uongozi. Ni jukumu letu kuendeleza juhudi hizi na kuwasaidia wengi waliokosa nafasi sawa,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji Barke Sehel alisema mbio hizo zikiwa na kaulimbiu “Mshikamano katika haki za kijinsia huanzia hapa: Shiriki na elimisha,” zinalenga kuhamasisha jamii kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Amesema maadhimisho hayo yatakayofanyika kwa siku kadhaa yatajumuisha kutembelea shule sita za sekondari ikiwamo ya Ilboru, Kimandolu, Kaloleni, Muriet na Sinoni na vilabu vya haki za kijinsia vitaanzishwa.

“Tutatoa elimu kuhusu aina za ukatili wa kijinsia, mbinu za kuripoti, na kuwapa wanafunzi ujuzi wa maisha kama vile kuweka malengo na kujali afya zao,” amesema Jaji Sehel.

Amesema maadhimisho hayo pia ni fursa ya kujivunia mafanikio makubwa ya TAWJA katika kukuza haki za binadamu, usawa wa kijinsia, na kuleta mchango chanya kwa jamii.

Jaji Sehel ametoa mfano wa juhudi za TAWJA zilizochangia kuboreshwa kwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa kuingiza kifungu maalumu kinachohusu rushwa ya ngono.

“Hii ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa jamii yenye haki na usawa kwa wote,” amesema

Related Posts