Spika wa Bunge la Tanzania Dokta Tulia Akson awakilishwa vyema Mbio za Miaka 25 ya TAWJA dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Na Jane Edward,Arusha

Spika wa bunge la Tanzania Dokta Tulia Akson amekipongeza chama cha majaji na mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA)kwa kuanzisha vilabu vya haki ya kijinsia katika shule sita za sekondari jijini Arusha kwani vilabu hivyo vitakuwa ni chachu ya kujenga hisia na kupandikiza mbegu ya kuamini na kusimamia haki katika jamii hapa nchini.

Akizungumza katika zoezi la mbio maalumu zilizoshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wanariadha,majaji,mahakimu,ikiwa ishara ya Maadhimisho ya jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake ,kwa niaba ya spika wa Bunge la Tanzania,Mwenyekiti wa mabunge wanawake Tanzania (TWPG)Shally Raymond amesema ana imani matokeo chanya ya mbio hizo zitainua hari kwa wananchi juu ya vitendo vya ukatili.

Amesema kuwa mbio hizo ni sehemu za harakati zinazolenga kuleta mabadiliko,kuzindua uelewa na kupinga masuala ya ukatili wa kijinsia (GBV)yaliyoshamiri na kukithiri katika jamii kwakuwa yamekuwa yakileta changamoto kwa wananchi. 

Ametoa rai kwa TAWJA kuwa pamoja na kujivunia mafanikio ni vyema pia ikatafakari kwa pamoja changamoto zinazoikabili jamii kwa kuwa bado kuna mila,tamaduni na mifumo gandamizi na nyingi zikiwa zimepitwa na wakati  ingawa wanawake na watoto bado wapo nyuma katika kutetea ma kulinda haki zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWJA, Barke Sehel, alibainisha kuwa maadhimisho ya miaka 25 yana kaulimbiu isemayo “Mshikamano katika Haki za Kijinsia Huanzia Hapa: “Shiriki na Elimisha.”  .” na kwamba mipango ya kutoa elimu, kukuza motisha, na kujenga uelewa wa pamoja wa haki za kijinsia,sanjari na hatua za kupambana na ukatili wa kijinsia.

Sehel aliongeza  kuwa wanachama wa TAWJA watatembelea shule sita zilizolengwa ili kuanzisha vilabu vya kutetea haki za kijinsia na kwamba vilabu hivyo vitajikita katika kuwaelimisha wanafunzi kutambua aina zote za ukatili wa kijinsia, kuelewa wapi pa kuripoti matukio hayo, kuweka malengo binafsi, na kuweka vipaumbele vya afya zao.

“Dhamira yetu ya kutetea haki na kukuza usawa wa kijinsia umejikita katika kutetea na kuendeleza haki za wanawake, watoto na makundi maalum nchini Tanzania,” Sehel alisema.

kupitia mipango hii, TAWJA inalenga kukuza utamaduni wa uelewa na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha mazingira salama na ya usawa kwa vizazi vijavyo.

Mwisho….

Related Posts