Mtoto aliyeibwa Januari 15 apatikana kwenye mashamba ya miwa

Kilosa. Mtoto Shamimu Nasibu, mwenye umri wa miaka miwili ambaye aliripotiwa kupotea alipokuwa akicheza na mwenzake karibu na nyumbani kwao, hatimaye amepatikana akiwa hai kwenye mashamba ya miwa katika Kijiji cha Kisanga, kata ya Ruaha, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Mtoto huyo aligunduliwa na wasamaria wema waliokuwa wakipita katika mashamba hayo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Jnuari 19, 2025, baba mzazi wa mtoto huyo, Nasib Ndihagule amesema Shamimu alipatikana akiwa hana nguo, hali inayozua maswali kuhusu nani alimvua nguo hizo na kwa sababu gani. Ameongeza kuwa baada ya kupatikana, mtoto alichukuliwa na polisi pamoja na viongozi wa serikali ya kijiji na kupelekwa katika kituo cha afya cha Kidodi kwa uchunguzi wa kitabibu ili kuhakikisha hali yake ya afya.

“Nilipigiwa simu leo asubuhi na watu waliomuona mtoto wangu kwenye mashamba ya miwa. Nilipofika huko, nilithibitisha kuwa ni mwanangu, ingawa nilishtushwa kumkuta akiwa hana nguo. Hali ya afya yake itajulikana baada ya uchunguzi wa daktari kukamilika,” amesema Ndihagule.

Amesema familia yake imepitia kipindi kigumu cha siku nne tangu mtoto huyo aliporipotiwa kupotea, lakini wanamshukuru Mungu pamoja na juhudi za Jeshi la Polisi, viongozi wa Serikali, na wananchi waliosaidia kuhakikisha Shamimu anapatikana akiwa hai.

Kuhusu tukio hilo, mama mzazi wa Shamimu, Halima Omary, amesimulia kwamba siku ya tukio, mtoto wake alikuwa akicheza nyuma ya nyumba yao na mwenzake.

Lakini akawahamishia mbele ya nyumba ili aweze kuwaona vizuri wakati akiendelea na shughuli zake za nyumbani.

“Niliwaweka kwenye kivuli cha mwembe mbele ya nyumba na wakati nikiwa ndani, nilikuwa natoka mara kwa mara kuwatazama. Mara ya mwisho nilipotoka, nilimkuta mwenzake peke yake Shamimu hakuwepo. Tangu siku hiyo, jitihada za kumtafuta zilianza mpaka leo alipopatikana,” amesema Halima.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema kupitia taarifa rasmi kuwa mtoto huyo alitelekezwa na watu wasiojulikana katika mashamba ya miwa kwenye kitongoji cha Mhovu yaliyopo Kijiji cha Kisanga.

Kamanda Mkama pia amebainisha kuwa mtu mmoja ambaye ni mganga wa jadi, anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hilo.

Katika hatua ya kujifunza kutoka kwa tukio hili, baba mzazi wa Shamimu amesema familia yake imepanga kuongeza umakini mkubwa katika kumlinda mtoto wao, ambaye bado hajaanza kuzungumza.

Related Posts