KOCHA wa Simba, Fadlu Davids ameonyesha kufurahishwa na viwango vya wachezaji wa timu hiyo na kuwamwagia sifa kutokana na kuonyesha ukomavu na kupata matokeo ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya CS Constantine ya Algeria wakati wakihitimisha mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba ilipata ushindi huo jioni ya leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam bila ya kuwepo kwa mashabiki wa klabu hiyo kutokana na adhabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) iliyoifungia timu hiyo kwa kosa la kufanya fujo na kuvunja viti mara baada ya mechi ya ushindi wa 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia mwishoni mwa mwaka jana.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, kocha Fadlu amesema ushindi huo ni ushirikiano wa benchi la ufundi, wachezaji na viongozi hivyo wametimiza malengo yao ya kuongoza kundi A kwa pointi 13.
“Tumecheza na timu nzuri, Ina kocha mzuri niwapingeze kwa kufanya vizuri hadi kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali haikuwa kazi rahisi. Jambo la msingi wachezaji wangu wameonyesha ukomavu wa kuamua matokeo ya ushindi, nafahamu mashabiki watakuwa wamefurahia hilo,” amesema Fadlu na kuongeza; “Kwa sasa tunataka kuweka nguvu kufanya vizuri ili kuweza kufika fainali.”
Kwa upande wa kocha wa Constantine, Kheireddine Madoui ameipongeza Simba kwa ushindi walioupata nyumbani, akisema amestahili kutokana na kiwango walichokionyesha.
“Kipindi cha kwanza tulijitahidi kuidhibiti Simba lakini kipindi cha pili kilikuwa kizuri kwao, baada ya kufungwa bao moja wachezaji wangu walipoteza umakini ikawa nafasi nzuri kwao kutufunga bao la pili,” amesema kocha huyo aliyewahi kuwindwa na Yanga mara ilipoachana na Miguel Gamondi na kuishia kumnyakua Sead Ramovic.
Timu hizo zote mbili zilishafuzu mapema hatua ya robo fainali na mechi ya leo ilikuwa ni ya kuamua ipi ikae kileleni na ipi ya kumaliza nafasi ya pili zikiungana na watetezi Zamalek ya Misri, RS Berkane ya Morocco na USM Alger ya Algeria zilizoongoza makundi mengine matatu, sambamba na Stellenbosch ya Afrika Kusini.
Nyingine tatu za kukamilisha idadi ya timu nane za kucheza hatua hiyo, inasubiri matokeo ya mechi za usiku huu za makundi ya B, C na D ambapo timu za Jaraaf ya Senegal, Enyimba ya Nigeria, Al Masry ya Misri na Asec Mimosas ya Ivory Coast zipo katika nafasi nzuri za kukata tiketi kama zitachanga vyema karata zao.