Dk Nchimbi mgombea mwenza urais CCM, hii hapa historia yake

Dodoma. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mgombea urais, Samia Suluhu Hassan amempendekeza Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2025.

Dk Nchimbi ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM Januari 15, 2024 katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kilichofanyikia Unguja, visiwani Zanzibar.

Dk Nchimbi alichukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo aliyejiuzulu Novemba 29, 2023.

Rais Samia amempendekeza Dk Nchimbi leo Jumapili, Januari 19, 2025 katika mkutano mkuu maalumu jijini Dodoma ulioanza jana Jumamosi. Ni mkutano huo huo umemchagua kwa kura za ndio 1924 sawa na asilimia 100 Samia kuwa mgombea urais.

Akitoa maelezo, Rais Samia amesema: “Kutafuta mgombea mwenza, lakini kama mnavyojua Dk Philip Mpango ndio Makamu wa Rais, amekuja kuniona kuniomba nimpumzishe, ana sababu kadhaa lakini sio za mahusiano ya kazi.”

“Anasema yeye ana miaka 68, angependa kuishi zaidi, ikiwezekana angonge 90 huko, akasema mama yake amefika 80 na, nilimbishia mbishia, wiki iliyopita akanikabidhi barua hii. Na barua sikumjibu. Nilipokwenda kuzungumza na kamati kuu tukakubaliana tumpumzishe.”

“Lakini nataka niwaambie, mambo tuliyoyaona pale yanapita pita ni kwa msaada wake, nimemtuma sana. Kwa kweli baada ya maelezo yake na kueleza katika kamati kuu, kumshukuru san asana kwa kazi aliyotufanyia na atakavyoebndelea ndani ya mwaka mmoja. Lakini bado yupo, ana miaka 68 tu, nitaendelea kumtumia.”

Rais Samia: “Sasa baada ya kupata barua ya Makamu wa Rais, tukahangaika kutafuta, tukaanza kufikiria nani anaweza kunisaidia, Marais watatu wastaafu Jakaya Kikwete, Aman Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein kunong’ona nao kuangalia labda waliokuwa nafikiri na wote tukakubaliana na jina moja.”

“Jina moja hilo ndilo nimelipeleka kamati kuu na wao wamelikubali, nalileta kwenu jina la kijana wenu Dk Emmanuel Nchimbi,” amesema Rais Samia huku ukumbi ukilipuka kwa shangwe.

Dk Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya. Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986.

Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.

Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

Dk Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.

Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).

Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.

Alisoma shahada ya uzamili ya usimamiz wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).

Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003–2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Dk Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.

Dk Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu.

Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.

Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.

Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013 kwa shinikizo, baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli juu ya “Oparesheni Tokomeza”.

Wakati watu wengi wanadhani Nchimbi aling’olewa uwaziri kwa shinikizo la Bunge, ukweli ni kuwa aliondoka kwa shinikizo la vikao vya CCM, “party caucas.”

Ripoti ya kamati ya Lembeli ilieleza wazi kuwa anayepaswa kuwajibishwa ni waziri mmoja tu (Dk Mathayo David, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) lakini “caucas” ya CCM ikawaangushia mzigo wengine watatu akiwamo Dk Nchimbi.

Lembeli aliwahi kukaririwa akisema: “Ripoti ilimtaja Dk Mathayo na sababu tulitoa mle ndani. Hao wengine watatu si kamati, ni mambo ya hukohuko kwenye party caucas. Ndiyo maana mara ya mwisho nilikwenda pale nikasema kuwa (Khamis) Kagasheki (Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, anaonewa.”

Machi mwaka 2017, akiwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Dk Nchimbi aliwahi kukumbwa na msukosuko ndani ya chama chake, akapewa onyo kali na adhabu ya kutogombea nafasi yoyote kwa kipindi cha miaka minne.

Adhabu hiyo ilitokana na kilichoelezwa na CCM kuwa, ni usaliti katika uchaguzi wa mwaka 2015. Hata hivyo, makada wengine wa chama hicho walifutwa uanachama akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba.

Katika uchaguzi huo, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kumpendekeza Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.

Dk Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba walikuwa wanamuunga mkono Edward Lowassa aliyekuwa akiwania urais mwaka 2015 kupitia CCM kabla ya jina lake kukatwa na kutimkia Chadema.

Hata hivyo, baada ya mgombea urais kupatikana, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani na kueleza kwamba kama chama kimefanya uamuzi, mtu akiendelea kuupinga, huo ni usaliti.

Related Posts