DODOMA Jiji imegoma kumuachia kirahisi mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Paul Peter aliyekuwa akitakiwa na Al Dahra ya Libya na kuwaita mezani Waarabu hao wakiwa na mzigo wa maana kama kweli wanataka kumbeba nyota huyo.
Timu hiyo ya Ligi Kuu Bara, inadaiwa imechomoa mara mbili ofa za Al Dahra iliyopo Ligi Kuu ya Libya zilizokuwa na kiwango kidogo cha fedha.
Inaelezwa, klabu hiyo ya Libya ilianza kutoa ofa ya Sh17 milioni na ilipobaniwa inaongeza hadi kufikia Sh25 milioni, lakini mabosi wa Dodoma Jiji waliamua kuzitupilia mbali kutokana na kuona ni kama dharau flani kwao kwa uwezo alionao nyota huyo mwenye mabao manne katika Ligi Kuu hadi sasa.
“Ni kweli Paul Peter amepata ofa kutoka Libya na ameshakubaliana nao kila kitu katika malipo binafsi, lakini fedha zilizoletwa kwa klabu zimeonekana ni ndogo, ndiyo maana tunataka waje vingine tuone kama tunaweza kumuachia, aende akacheze soka la kulipwa humo,” mmoja wa vigogo wa Dodoma Jiji alifichua.
Mkataba wa nyota huyo wa zamani wa Azam FC na KMC unamalizika mwisho wa msimu huu na kwa sasa unaelezwa umesaliwa na muda wa miezi mitano, ndiyo maana Al Dahra ilifanya mazungumzo na Dodoma Jiji pamoja na menejimenti ya mchezaji huyo ili imbebe.
Taarifa nyingine zinasema, dau la usajili alilowekewa mchezaji huyo mezani ni zaidi ya Sh100 milioni na iwapo Dodoma Jiji itaamua kuridhia asepe atakuwa amepiga hela ya maana kabla ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo inayoburuza mkia katika Kundi la Nne la Ligi Kuu ya nchi hiyo ikiwa na pointi mbili tu, licha ya kucheza mechi sita hadi sasa ikipoteza mechi nne na kutoka sare mbili, huku ikiwa haina ushindi wowote. Al Dahra inamtaka nyota huyo wa Dodoma ili kwenda kuiokoa, kwani katika mechi hizo sita ilizocheza haijafunga bao lolote licha ya yenyewe kuruhusu mabao manane hadi sasa.
Dodoma inayonolewa na kocha Mecky Maxime ipo nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu, ikicheza mechi 16, ikishinda tano kutoka sare nne na kupoteza saba ikivuna pointi 19 na kufunga mabao 16 na kufungwa 25, huku Paul Peter akiwa ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa na manne, akifuatiwa na kinda aliyetua Azam FC, Zidane Sereri (matatu).