Mastaa wamkosha Mfaransa Singida Black Stars

KOCHA wa Singida Black Stars, Mfaransa Miloud Hamdi amesema hadi sasa kikosi hicho kiko katika mwelekeo mzuri ingawa ana kazi kubwa ya kufanya kwenye mzunguko huu wa pili wa Ligi Kuu Bara, kutokana na ushindani mkubwa uliopo kwa kila timu.

Kocha huyo mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Algeria aliyeteuliwa Desemba 30, mwaka jana, amezungumza hayo baada tu ya kuridhishwa na viwango vya wachezaji, tangu achukue nafasi ya Mbelgiji Patrick Aussems aliyeondoka Novemba 29, mwaka jana.

“Tuko katika mwelekeo mzuri lakini tuna kazi kubwa ya kufanya mzunguko wa pili ili kuendana na ushindani, naamini kwa kikosi kilichopo na maboresho tuliyoyafanya, tutatimiza malengo yetu ya kushikilia tulipo au kusogea juu zaidi.”

Kocha huyo aliongeza, jambo zuri kwao kwa sasa hawana mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara hivyo, inampa nafasi ya kuendelea kukisuka vyema kikosi hicho kwa michezo ijayo, huku akijivunia morali na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji.

Hamdi aliyezaliwa Juni Mosi, 1971, huku akipenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 katika timu mbalimbali alizofundisha, alikuwa hana timu yoyote tangu alipoachana na Al-Khaldiya FC ya Bahrain, aliyoifundisha Julai Mosi, 2023 hadi Desemba 13, 2023.

Kocha huyo mbali na kuifundisha Al-Khaldiya FC, timu nyingine alizowahi kuzifundisha ni USM Alger na JS Kabylie za kwao Algeria, Al-Salmiya ya Kuwait, Athletico Marseille na ES Vitrolles za Ufaransa na Al-Ettifaq FC (U-23) kutoka Saudi Arabia.

Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida, Hussein Massanza alisema baada ya Ligi Kuu Bara kurejea Februari, tayari wanajiandaa kurudi mjini Singida kwa ajili ya kuendelea na programu mbalimbali ili kujiweka fiti kwa mashindano.

“Awali tulipanga tukae takribani mwezi mzima hapa Arusha lakini baada ya taarifa za ligi kurejea Februari, tumeamua kusitisha kambi yetu kwa muda huo na sasa tutarudi Singida na kupata michezo ya kirafiki angalau miwili tu,” alisema.

Related Posts