Watafiti wametakiwa kushirikisha makundi mbalimbali ya jinsia zote katika hatua za awali za utafiti wao ili kupata taarifa zitakazoisadia Serikali kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii pamoja na kupanga mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Wito huo umetolewa na Mkurugeni wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Devotha Mosha kwenye warsha ya kuwajengea uwezo watafiti wachanga katika ukusanyaji na uchakataji wa takwimu ili kupata tafiti zilizo bora zenye manufaa kwa jamii, taasisi na taifa kwa ujumla.
Dkt. Devotha ambaye pia ni Kiongozi wa Kitengo cha Jamii katika masuala ya jinsia kwenye Mradi wa Utafiti wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY) amesema watafiti wanatakiwa kutumia mbinu shirikishi na kushirikisha makundi yote wakiwemo wanawake, wanaume, wazee, vijana, matajiri, maskini na makundi mengine ili kupata taarifa zitakazogusa makundi yote kwenye jamii.
“Kama mnavyojua bila mbinu shirikishi huwezi kupata taarifa zilizo sahihi ambazo zinajitosheleza katika kutoa mapendekezo mbalimbali katika taasisi zetu na kwa Serikali pia, hivyo nitumie fursa hii kutoa wito kwa watafiti wanaposikia kuna mafunzo ya aina hii wajitahidi kushiriki kwa wingi ili kuja kujifunza na kujiendeleza ikiwa ni pamoja na kuzijua hizi mbinu shirikishi ambazo zina faida kwa jamii”, amesema Dkt.Devotha.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo akiwemo Egata Makanja kutaka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Rehema Mollel Mkufunzi Msaidizi, Idara ya Maendeleo na Mafunzo ya Kimkakati kutoka SUA wameupongeza mradi wa CLARITY kwa kuandaa warsha hiyo ambayo imekuwa na faida kubwa kwao.
“Pale NDC tuna miradi mingi ya maendeleo hivyo mafunzo haya yatanisaidia kufanya tafiti mbalimbali ili kupata taarifa zilizo bora ambazo tutazichakata na kuzisambaza kwa jamii kwa matumizi mbalimbali”, amesema Makanja.
“Nimefurahi sana kupata nafasi hii kwa sababu nilikuwa natamani kujifunza kwa muda mrefu, japokuwa tumejifunza darasani lakini haikuwa kwa uwanja mkubwa kama tulivyofundishwa hapa, naona kabisa mafunzo haya yameniongezea maarifa katika utendaji wa kazi zangu”, amesema Rehema.
Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yamedhaniniwa na Mradi wa CLARITY yamewakutanisha pamoja washiriki 70 na wengine zaidi ya 100 wameshiriki kwa njia ya mtandao ambapo wote wamepewa vyeti vya ushiriki.