Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa, alisema tuzo hizo zinadhihirisha juhudi za dhati za kuboresha maisha ya wafanyakazi wake ndani na nje ya kazi.
“Tuzo hii ni ishara ya wazi kwamba Benki ya CRDB inajali na kuthamini wafanyakazi wake, ikiwapa mazingira bora yanayowezesha mafanikio yao binafsi na ya kitaaluma. Huu ni ushindi wa pamoja, si wa benki pekee bali pia ni wa familia nzima ikiwamo wateja na wadau wote wa Benki ya CRDB,” amesema.
Tuzo ya Top Employer inatolewa baada ya tathmini ya kina ya viwango vya usimamizi wa rasilimali watu, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika maendeleo ya kitaaluma, usawa wa kijinsia, programu za afya na ustawi wa wafanyakazi, na utamaduni wa uwazi na mshikamano. Katika maeneo haya, Benki ya CRDB imeonyesha ubora wa kipekee, ikiwasaidia wafanyakazi wake kufanikisha ndoto zao za kitaaluma huku wakichangia ukuaji wa Benki hiyo kwa kasi.
Tuzo za Top Employer ni mwendelezo wa Benki ya CRDB kutambuliwa kimataifa ambapo katika mwaka 2024 pekee, Benki hiyo ilikusanya tuzo zaidi ya 50 za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Benki Bora Tanzania, huduma bora kwa wateja, ubora wa huduma za kidijitali, na ufanisi wa mikakati ya maendeleo endelevu. Tuzo ya Top Employer ni nyongeza ya heshima inayodhihirisha dhamira ya benki hiyo ya kuimarisha rasilimali watu kama msingi wa mafanikio yake.
Rutasingwa alibainisha kuwa Benki ya CRDB inajipanga kuimarisha nafasi yake kama kinara wa usimamizi wa vipaji barani Afrika. “Tunajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko yanayoangazia wafanyakazi kama rasilimali muhimu. Maendeleo endelevu ya benki yetu hayawezekani bila jitihada za kila mfanyakazi,” aliongeza.
Rutasingwa alitoa wito kwa wafanyakazi wa benki hiyo kuendelea kuonyesha moyo wa ushirikiano na ubunifu, akisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja. “Benki ya CRDB si tu sehemu ya kazi – ni familia inayowekeza katika ndoto na ustawi wa kila mmoja wetu. Ushindi huu unathibitisha dhamira yetu ya kuweka viwango vipya vya ubora,” alisema.
Kupitia tuzo hizo za Top Employer, Rutasingwa amewahakikishia wadau, wateja, na washirika wa Benki hiyo kuwa itaendelea kuwekeza katika ubora wa wafanyakazi wake, lakini pia katika huduma na bidhaa ili kukuza ustawi wa watu wake na jamii kwa ujumla.