WAKATI Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, Fiston Mayele akikwama kufika japo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, akiwa na Pyramids ya Misri anayoicheza kwa sasa, nyota mwenzake wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda ametumia dakika 30 tu, kufika fainali nyingine ya Shirikisho na sasa anajiandaa kubeba taji akiwa RS Berkane ya Morocco.
Mayele aliyemaliza hatua ya makundi akiwa mabao mawili na asisti moja wakati Pyramids ikimaliza mkiani mwa Kundi A ikiziacha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na TP Mazembe ya DR Congo zikivuka robo, lakini kwa Kisinda mambo yameonekana mepesi mno.
Mayele alifunika msimu uliopita akifunga mabao saba ya Kombe la Shirikisho akiwa ndiye kinara na mengine saba katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Yanga iling’olewa raundi ya kwanza na Al Hilal ya Sudan, pia akiwa ndiye kinara wa Ligi Kuu Bara akifunga 17 akilingana na Saido Ntibazonkiza wa Simba.
Cha kushtua ni kwamba, Kisinda ametumia dakika 30 za msimu huu wa Kombe la Shirikisho hadi mchezo wa kwanza wa fainali.
Hii ni fainali ya tatu mfululizo kwa Kisinda, kwani awali alifika na kubeba taji 2022 akiwa na Berkane kabla ya Yanga kumnyakua na kucheza nao fainali ya msimu uliopita iliyopoteza mbele ya USM Alger na sasa ametinga tena na Berkane iliyotoka kuifumua Zamalek ya Misri kwa mabao 2-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza.
Mayele na Kisinda ni baadhi ya wachezaji walioifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini mbele ya USM Alger baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.
Yanga ilifungwa nyumbani 2-1 na kushinda ugenini kwa bao la penalti ya beki Djuma Shaban ambaye hayupo katika timu hiyo kwa sasa kama ilivyo kwa kina Kisinda waliondoka klabu hapo mwishoni mwa msimu uliopita.
Kisinda aliyerejeshwa Berkane baada ya kuichezea Yanga kwa mkopo msimu uliopita, ametumika katika mechi tatu tu hadi sasa za msimu huu za Kombe la Shirikisho akiwa na timu hiyo iliyomaliza kinara wa Kundi D, ikivuna jumla ya pointi 14 kupitia michezo sita ya makundi.
Winga huyo alianza kutumika wakati Berkane ikivaana na Sekhukhune ya Afrika Kusini iliyomkutanisha na nyota wenzake wa zamani wa Yanga, Michael Sarpong na mchezo kuisha kwa suluhu, huku Wasauzi waliokuwa wenyeji akimaliza pungufu baada ya Jamie Webber kulimwa kadi nyekundu dakika ya 41 tu ya pambano hilo, lililoifanya Berkane kufikisha pointi 11 kundini.
Katika mchezo huo, Kisinda aliingizwa dakika ya 76 kumpokea Youssef Mehri, kisha akacheza katika mechi ya kuamua kinara wa kunfi wakati Berkane ikivaana na Stade Malien ya Mali, aliingizwa dakika ya 90 kuchukua pia nafasi ya Mehri wakati huo kikosi cha timu hiyo ya Morocco ikiwa imeshajihakikishia ushindi wa mabao 3-0, matokeo yaliyoifanya imalize kama kinara wa kundi hilo mbele ya Malien iliyomaliza ya pili na pointi 10.
Kwa mujibu wa rekodi ni kwamba Kisinda alitumika kwa dakika 16 tu katika mechi za makundi hadi timu kutinga robo fainali. Katika mechi za robo fainali dhidi ya Abu Salim ya Libya ambapo Berkane ililazimisha suluhu ugenini na kushinda nyumbani mabao 3-2, Kisinda aliishia kukaa benchi na katika mechi za nusu fainali ambazo hazikuchezewa kutokana na USM Alger kuleta siasa mchezoni, ilimlainishia winga huyo kutinga fainali.
Katika mechi ya kwanza ya fainali iliyopigwa wikiendi iliyopita, Kisinda alitumika kwa dakika 14 tu, baada ya kuingizwa akitokea benchi dakika ya 76 akimpokea Mohamed El Morabit aliyeasisti bao la pili lililofungwa na Adil Tahif na kumfanya hadi fainali hiyo awe amecheza kwa dakika 30 tu bila ya bao wala kuasisti, lakini akijindaa kutwaa taji la pili la CAF.
Zamalek wikiendi hii itakuwa wenyeji wa fainali ya pili na kama matokeo yataisha kwa kuibeba Berkane.
Kishinda aliyewahi kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021-2022 akiwa na kikosi hicho Berkane kilichomnunua kutoka Yanga, kwa sasa anasikilizia tu kuona mechi hiyo ya wikiendi itakuwa na manufaa gani kwa Berkane ili aendelee kuboresha ‘cv’ yake katika soka la kimataifa, licha ya kwamba hatumiki katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo tangu arejee kikosini.
Rekodi zinaonyesha kuwa, Kisinda ametumika kwenye mechi 22 hadi sasa akiwa na Berkane, tatu zikiwa Kombe la Shirikisho alizatumika kwa dakika 30 na mechi nyingine saba akiishia kukaaa becnhi katika michuano hiyo ya CAF, michezo mingine 14 ikiwa ni ya Ligi Kuu ya Morocco (Batola Pro).
Katika mechi hizo za 14 za Ligi, tano aliishia kukaa benchi, huku tisa pekee akitumikwa kwa jumla ya dakika 292 ambapo ni mchezo mmoja tu dhidi ya Moghreb Tetouan ndio alitumika kwa dakika zote 90, japo hana bao wala asisti yote hadi sasa katika ligi hiyo inayoelekea ukingoni.
Berkane, tayari inamiliki mataji mawili ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwani awali ilitwaa mwaka 2020 kabla ya kurudia tena ikiwa na Kisinda mwaka 2022 ambapo pia ilibeba taji la CAF Super Cup ikiwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha aliyeachana na Simba hivi karibuni.
Hii ni mara ya nane kwa timu hiyo kushiriki michuano hiyo tangu 2015 na kama itafanikiwa kulinda ushindi wake wa nyumbani dhidi ya Zamalek wikiendi hii jijini Cairo, itaiwezesha kutwaa kwa mara ya tatu na kulingana na vinara wa sasa wa michuano hiyo, Club Sfaxien ya Tunisia.