Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kuelekea mkutano mkuu wa chama hicho kesho, ni nafasi ya kuionyesha dunia wanavyoweza kujijenga ndani ya tofauti zilizopo.
Amesema watu wengi wanaiangalia Chadema, wakiwemo wale wa macho ya husda na wivu na wangetamani kuona mkutano huo unaisha huku chama hicho kikiwa vipandevipande.
Mbowe ameyasema hayo leo, Jumatatu Januari 20, 2025 alipofungua mkutano wa baraza kuu la chama hicho ulilofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Amesema kwa sasa karibu dunia inaiangalia Chadema na ndani yake yapo macho ya husda na wivu akidai kuwa wapo wanaotamani kukiona chama hicho kikiondoka Mlimani City kikiwa vipande vipande na kwamba watashindwa.
“Tumekuja Dar es Salaam sio kupaniana, tumekuja kuyajenga kwamba chama hiki tutakijenga, tutakipanga ili mwisho wa siku chama chetu kibebe ndoto za Watanzania,” amesema.
Amesema ni muhimu kuionesha dunia kuwa chama hicho ni kikubwa kuliko tofauti zao.
Mbowe amesema matumaini ya wajumbe wote waliofika ukumbini hapo watatoka ukumbini wakiwa wamoja.
Amesema wasitoe nafasi kwa yeyote anayetaka kukipasua chama hicho na wanapaswa kuonyesha namna wanavyoweza kuijenga taasisi ndani ya tofauti zao.
“Siku ambayo dunia nzima inasubiri, watesi wetu wanaisubiri, marafiki zetu wanaisubiri, twendeni tukawaonyeshe kwamba Chadema ni mpango wa Mungu,” amesema.
Amesema chama hicho kitaendelea kuwa familia, pamoja na mivutano midogomidogo iliyopo.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema amesema baraza linalofanyika leo, ndilo lenye mamlaka ya uteuzi wa wagombea wa uenyekiti na makamu wake.
“Usije kushangaa wagombea wa uenyekiti wakabaki wachache kwa kuwa baraza kuu la leo ndilo lenye mamlaka ya kuteua,” amesema.
Baada ya uteuzi huo, amesema kesho wagombea hao watapigiwa kura katika mkutano mkuu wa chama hicho ambao ratiba yake itaanza saa 5:00 asubuhi na.
Ameeleza wageni zaidi ya 50 watashiriki mkutano huo wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali na viongozi wa kisiasa kutoka nje.
Amesema Januari 22, mwaka huu utafanyika uchaguzi wa wajumbe wanane wa kamati kuu watakaochaguliwa na baraza kuu na kisha kupendekezwa jina la katibu mkuu.