NBC yatoa vifaa tiba hospitali ya Mpitimbi Songea

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa misaada ya vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh. 11.5 milioni kusaidia kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Mpitimbi, Songea Mkoani Ruvuma. Vifaa hivyo ni kitanda cha kujifungulia 1, vitanda vya wagonjwa 15, magodoro 15, madawa na vifaa tiba. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Vifaa tiba hivyo vimekabidhiwa jana Jumatatu kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi Gilbert Donatius Simya aliepokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki ya NBC Elibariki Masuke (wa tatu kushoto) akikabidhi sehemu ya msaada wa vifaa tiba kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Gilbert Simya ili kusaidia kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Mpitimbi, Songea Mkoani Ruvuma.

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika hospitalini hapo jana ikihusisha viongozi waandamizi wa mkoa na hospitali hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea, Elizabeth Gumbo na Padre wa Jimbo Kuu la Katoliki la Songea Padre, Wilhem Soni.

Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki ya NBC, Elibariki Masuke aliwaongoza maofisa wengine wa benki hiyo kukabidhi msaada huo.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo, Masuke alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini huku pia ikiwajibika kupitia sera yake ya kusaidia jamii hususani kwenye suala zima la kuboresha afya ya jamii.

“Benki ya NBC tunaamini katika kuboresha afya ya mama na mtoto. Ni kutokana azma yetu hiyo leo tunakabidhi vifaa hivi ili kuchangia katika uboreshaji wa afya ya wananchi wa Mpitimbi, Songea tukitambua kuwa tunajukumu la kuchangia na kuinua mazingira ya jamii inayotuzunguka, lakini pia kujenga taifa imara lenye afya na nguvu,’’ alisema.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Gilbert Simya akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya kupokea msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na benki ya NBC ili kusaidia kuboresha huduma za afya katika Hospitali ya Mpitimbi, Songea Mkoani Ruvuma.

Masuke alitumia nafasi hiyo kutaja baadhi ya jitihada zinazofanywa na benki hiyo katika kuboresha sekta ya afya nchini kuwa ni pamoja na mbio za NBC Dodoma Marathon ambapo benki hiyo hukusanya fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake nchini.

“Kupitia mbio hizi tumeweza kuleta hamasa kwa wanawake 23,000 amabao kati yao zaidi ya 1090 wamekutwa na vimelea vya kansa hio na wameshapatiwa matibabu,’’ alitaja huku akiongeza;

“Vile vile kupitia mbio hizi pia tunatoa ufadhili wa mafunzo kwa wakunga 100 kwa kushirikiana na taasisi ya Benjamin Mkapa katika kuboresha afya na uzazi salama kwa mama na mtoto Tanzania. Tunajivunia kuwa mpaka sasa wakunga 50 wameshapatiwa mafunzo na wameweza kurudi kazini wakiwa na ujuzi zaidi wa kuokoa maisha ya mama na mtoto.’’

Aliongeza kuwa benki hiyo imedhamini na kuratibu NBC mobile clinics ambazo ni kliniki zinazotembea katika visiwa vya Zanzibar katika kuboresha afya za wananchi katika sehmu mbalimbali visiwani humo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhandisi Simya aliishukuru benki ya NBC kwa msaada huo huku akielezea namna msaada huo utakavyosaidia kuboresha huduma ya afya hospitalini hapo kutokana na wingi wa wagonjwa wanaofika kupata huduma hospitalini hapo.

“Msaada huu utakuwa na tija kubwa sana kwa wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapa wakiwemo wakazi wa hapa na maeneo Jirani. Licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali katika kuboresha huduma za afya bado zinahitajika juhudi za wadau mbalimbali kufanikisha jitihada hizo…hivyo nawaomba sana wadau kama NBC muendelee kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika uboreshaji wa sekta mbalimbali ikiwemo hii ya afya,’’ alisema.

Kwa upande wake Padre Wilhem Soni aliishukuru NBC kwa msaada huo akibainisha kuwa Hospitali hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa wengi wakiwemo wale wanaohitaji huduma ya kulazwa pamoja na huduma ya uzazi hivyo msaada wa vitanda hivyo pamoja na vifaa tiba vingine vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuwahudumia wagonjwa hao.

Related Posts