Na; Mwandishi Wetu – DODOMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhishwa na utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake namna inavyowagusa wananchi na kumpongeza Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kukuza ustawi na maendeleo ya Watanzania.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq leo Januari 21, 2025 Jijini Dodoma wakati wa kikao cha kamati ikipokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024.
Aidha, Mhe. Toufiq ameshauri taasisi hizo zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kuongeza wigo wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini ili kusongeza huduma karibu na wananchi.
Vile Vile, amepongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali wa usimamizi na uendeshaji wa mashauri (Online Case Management System) utasaidia kuongeza ufanisi katika kusuluhusha na kuamua migogoro ya kikazi kwa urahisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Ofisi hiyo katika mwaka wa fedha 2024/2025 ilipanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo usimamizi wa kazi na huduma za ukaguzi, maendeleo ya vijana, kuratibu shughuli za ajira na utoaji huduma za ajira nchini, huduma kwa watu wenye Ulemavu, hifadhi ya jamii na ukuzaji tija, hivyo ameahidi kamati hiyo kuwa ofisi hiyo itatekeleza majukumu hayo ili kufikia malengo yaliyoweka.
Katika kikao hicho ameshiriki pia Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Mary Maganga, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Zuhura Yunus, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Abdul – Razaq Badru, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda.