NILILIONA pengo la Prince Dube katika pambano la Azam dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam Alhamisi jioni halafu baadaye ikawa usiku. Azam walikosa mabao kadhaa ya wazi katika pambano hilo.
Dube alikuwa wapi? sijui. Mara ya mwisho nilikutana naye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam. wote tulikuwa tunasafiri kwenda nchi tofauti lakini Ligi Kuu ya Tanzania bara ilikuwa inaendelea. Alikuwa na familia yake na sijui kama mke wake na watoto wake wanajua hasa ambacho baba yao anafanya.
Na sasa ni wazi kwamba Azam wanamhitaji mshambuliaji wao kuliko nyakati nyingine zozote zile. Kuna vita ya kuwania nafasi adimu ya pili kati ya Simba na Azam. Azam wanamkosa mmoja kati ya washambuliaji wao bora katika kipindi hiki.
Feisal Salum anafunga, lakini hawezi kufunga peke yake, kila mechi. Ni kama ambavyo Aziz Ki anafunga sana pale Yanga lakini hawezi kufunga peke yake na kila mechi. Uzuri ni kwamba pale kwa Aziz kuna watu wengine wanaomsaidia. Asingepofunga yeye Mudathir Yahya ama Joseph Guede au mtu mwingine atafunga.
Alhamisi jioni Dube ambaye ana rekodi nzuri ya kuifunga Simba alikosekana. Hakukuwa na bao la Feisal wala mchezaji yeyote wa Azam. wakacheza na KMC wakafunga mabao. Feisal hakufunga. Na sasa wanapambana kushinda mechi zao zote ili wacheze Ligi ya mabingwa barani Afrika. Wakati huo Dube anatazama mechi katika kochi. Ana mkataba na Azam mpaka mwisho wa msimu au miaka miwili mingine ijayo.
Mwenyewe anadai mkataba wake unafika mwishoni mwa msimu huu, hatujali sana. Ameshindwa kesi. Hata kama angeshinda kesi lakini si ni bado mchezaji wa Azam? alipaswa kuwepo uwanjani katika pambano dhidi ya Simba.
Hata hivyo Azam wanaumizwa kimya kimya na kilichotokea kwa Dube. Hawawezi kwenda hadharani kuelezea namna wanavyoumizwa na jambo hili kwa sababu na wao walifanya kitu kama hiki kwa Yanga. Akili ya Fei Toto ikageuzwa na kuwaacha Yanga wakiwa hawana mchezaji muhimu katika michuano ya Shirikisho, Ligi Kuu pamoja na michuano ya FA. Bahati nzuri walifanikiwa kufika mpaka mwisho wa kila michuano waliyokuwepo. Miwili walichuano na mmoja wakafungwa na USM Alger katika hatua ya fainali.
Azam nao wanalazimika kuishi hivi huku wakiwa na mkataba wa mchezaji mkononi. Wana michuano miwili mkononi. Kilichoenda ndicho walichorudishiwa. Nasikia usumbufu wake aliaunza muda mrefu hata hivyo nadhani alitiwa moyo zaidi wa kugoma pale alipogundua kwamba mwenzake Fei alikuwa ameshinda kesi yake kiulaini bila ya majibu ya CAS wala FIFA.
Pale ndipo tulipofungua mlango ambao ulisababisha Azam wamkose Dube siku ya Alhamisi. Lakini wanaendelea kumkosa na wataendelea kumkosa mpaka mwishoni mwa msimu huu. Ataendelea kuwa katika kochi akitazama mechi huku miguu yake ikiwa fiti.
Nina wosia kwa pande mbili. Kwanza kabisa wachezaji na mawakala wao wajitambue. Uhuni wa namna hii huwa unafanywa mwishoni mwa msimu. Unatoa fursa kwa klabu iliyoathirika kumnasa mchezaji mpya katika nafasi hiyo.
Wachezaji wa nchi za wenzetu zilizoendelea kisoka huwa wanafanya uhuni huu mwisho wa msimu. Utasikia mchezaji anaomba kuuzwa, utasikia mchezaji hajaripoti katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya. ili mradi tu afanye vurugu aondoke zake.
Wakati mwingine klabu inakuwa inabisha huku kichinichini ikianza maandalizi ya kuchukua mchezaji mwingine mkali wa kuziba nafasi yake. Dube hakuipa Azam nafasi hii ingawa angeweza kuipa. Kiungwana kabisa Azam walitaka pesa ili aondoke lakini tatizo halikuwa pesa. Pesa sio kila kitu. Tatizo ni mshambuliaji gani mkali atasimama pale mbele kuziba nafasi yake wakati msimu upo hai? Hakuna kanuni za usajili zinazowaruhusu Azam kuziba nafasi yake wakati Ligi inaendelea.
Lakini hapo hapo kwa wachezaji wenyewe. Wanapoteza ubora wao. Kama kweli Dube akienda Yanga itamchukua muda kidogo kuwa fiti katika kikosi cha kwanza. Kwa sasa anafanya mazoezi tu, lakini hawezi kuwa fiti kama ambavyo ingekuwa kama angekuwa anacheza mechi.
Tuliona kwa Fei. Alianza kunenepa. Akakosa ufiti. Akatugharimu katika mechi mbili za kimataifa kati ya Taifa Stars na Uganda. Kama Rais Samia Suluhu asingeingilia kati si ajabu mpaka leo Fei angekuwa Zanzibar akicheza na watoto huku akiwa amenenepa.
Wachezaji wetu wasiingezwe na mkenge wa katikati ya msimu na mawakala wao au timu zao zinazowataka. Wawe na subira kidogo pindi wanapotakiwa na klabu nyingine. Vurugu huwa zinafanywa wakati msimu unapofika tamati.
Lakini Shirikisho la soka nchini, TFF, lazima liongeze kanuni za adhabu kwa wachezaji ambao wanaanzisha vurugu katikati ya msimu. Kwa sasa unaweza kuwaelewa kwamba kanuni hazina meno kwao lakini kwa utoto huu unaoendelea nadhani kuna jambo lazima lifanyike.
Vinginevyo tunasubiri kesi nyingine kama hii itokee msimu ujao na kisha msimu mwingine. Lazima kuna jambo kama hili litatokea msimu ujao. Naambiwa kuna mchezaji mmoja wa Singida Fontain Gate amebeba mizigo na amekwenda kwao. Hana sababu ya msingi na mshahara anapokea kama kawaida.
Labda kwa sababu mchezaji huyo amepokea ofa ya mkataba wa timu kubwa ameamua kuingia zake mitini kwa sababu amepoteza hamu ya kuichezea timu yake. Je timu yake inalindwa na kanuni zipi katika mazingira kama haya.
Nani ataufunga mlango huu? Wachezaji, klabu au TFF? Na vipi ikitokea klabu haimuhitaji mchezaji fulani lakini inamlaghai kwa ajili ya kuhakikisha haendelei kutoa mchango wake katika klabu yake ili ushindani upungue?