Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe ametoa maagizo mawili kwa uongozi mpya wa chama hicho chini ya mwenyekiti mpya Tundu Lissu ya kuponya majeraha ya uchaguzi na kuilinda katiba ya chama.
Ametoa maagizo hayo leo Jumatano Januari 22 jijini Dar es Salaam baada ya kutolewa matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Lissu na makamu wake-bara, John Heche.
Mbowe ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Chadema atakuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu ametoa salamu zake kwa wajumbe wa mkutano mkuu katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam akisema: “Tumemaliza uchaguzi huu, lakini uchaguzi huu umeacha majeraha mengi kwa chama chetu, ushauri wangu kwa viongozi wetu kakiponyeni chama chetu.”
“Mimi niliahidi ningeshinda ningeunda tume ya ukweli na maridhiano, watu wakazungumze yaliyojiri kwenye uchaguzi huu, watu walipokoseana, walipokosana, walipokosa maadili, walipokibagaza chama chetu, wakasameheane wapeane mikono ili chama chetu kiwe na nguvu zaidi,” amesema.
Mbowe aliyekaa madarakani kwa miaka 21 akichukua kijiti kutoka kwa Bob Makani amesema: “Kama mnaniheshimu kama mtu niliyekifanyia kazi chama hiki, nawaagiza haraka kaundeni tume ya ukweli na upatabishi, mkatibu majeraha ili muweze kujenga umoja.”
“Ushindi wowote ni ushindi wa chama, asitoke mmoja wetu akaleta kiburi cha uchaguzi. Oneni ulazima wa kutibu majeraha ya mchakato wa uchaguzi.”
Mbowe pia, amewaasa viongozi wapya kuilinda katiba ya chama badala kuendesha chama kwa mapenzi yao.
“Tembeeni kwenye katiba ya chama, msitembee kwenye mapenzi yenu, tembeeni kwenye katiba. Pale mnapoona katiba ina upungufu, shirikisheni wenzenu.”
Akizungumzia mnyukano uliokuwepo katika uchaguzi huo, Mbowe amesema kuna watu walimshauri ajitoe lakini aliwakatalia.
“Wakati mnyukano umekolea wapo walioniambia toka, nikawaambia nitafia kwenye demokrasia. Naondoka nikiwa na fahari kwa demokrasia niliyoijenga kwa miaka 30,” amesema.
Amesema katika mazungumzo yake mbalimbali aliahidi uchaguzi huo utakuwa huru, wazi na wa kidemokrasia jambo ambalo kila mmoja ndani na nje ya Chadema na Tanzania wameshuhudia hilo.
Mbowe ameishukuru familia yake kwa kumvumilia kwa muda wote aliokuwa kiongozi wa Chadema.
“Baada ya matokeo, wa kwanza kunipigia simu alikuwa binti yangu, halafu akaja mama yake wakasema nirudi nyumbani wakanipikie supu, nikampa akaongea na Lissu. Sisi ni rafiki wa familia,” amesema.
Amesema kwa kuwa yeye ni mfanyabiashara, amepata likizo ya wafanyabiashara:”Nakwenda kutafuta mafekechee.”
Akizungumzia suala la kuponya chama hicho, mwenyekiti mpya, Lissu amesema makovu hayo ni ya muda mrefu na watayashughulikia.
“Wanachama wameumizwa, tunahitaji kuwapa matumaini mapya. Tuna kazi za kuwaponya, tuna kazi za kuwaambia walioenguliwa, tuwaambie haya mambo yaliyosababishwa na uchaguzi hayajirudii,” amesema Lissu.
“Tutakwenda kule yalipoanzia, tutawaridhisha waliokata tamaa, tutaombana msamaha, mimi ni mtu wa haki, mimi sio mtu wa visasi, tutaponya majeraha,” amesema.
Amesema kuna taratibu zilizoingizwa kwenye chama ambazo sio za kikatiba watazishughulikia.
“Tutahakikisha tunatengeneza utaratibu bora wa chaguzi zetu. Mimi ni mtu wa haki. Tutahakikisha kila mwanachama anayetaka kugombea nafasi yoyote, anagombea,” amesema.
Amegusia malalamiko ya makada walioenguliwa kwenye uchaguzi wa kamati kuu, akisema ataanza na malalamiko yao.
“Wamekata rufaa, tutasikiliza rufaa zao kama zina merit tutawarudisha. Kama itashindikana tutaahirisha uchaguzi huo, tutakwenda kuzungumza kwenye Baraza Kuu.
Hatuwezi kuzungumza mambo ya CCM wakati yetu sio mazuri. Toa kwanza boriti kwenye jicho lako ndipo ulione boriti kwenye jicho la mwenzako,” amesema.
Katika hatua nyingine, amempongeza Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika: “Ni mtu mwadilifu na msafi, nilivyomfahamu tangu siku ya kwanza hadi sasa hajawahi kubadilika. Amefanya kazi na mwenyekiti kwa miaka yote lakini amesimamia uchaguzi ukiwa umenyooka. Hakutaka kuona aibu na kupindisha mambo.”