Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema hatokuwa na ndimi mbili kwenye utumishi wake.
Lissu amesema hayo leo Jumatano, Januari 22, 2025 baada ya kushinda nafasi ya uenyekiti wa chama hicho akimbwaga aliyekuwa Mwenyekiti Freeman Mbowe.
Katika hotuba yake, Lissu amegusia masuala mbalimbali ambayo uongozi wake utayasimamia ikiwamo kushusha madaraka na kuweka ukomo wa uongozi.
Akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam amesema:”Tumelipata tukilokuwa tukilitafuta, sasa tufanye kazi na kazi inaanza leo. Kuanzia leo, kesho na siku zinazofuata tunafanya kazi ya kuhakikisha tunajenga chama chetu.”
Amesema moja ya kazi iliyopo ni kuleta jina la katibu mkuu wa Chadema saa tisa alasiri ya leo. Pia, jina la naibu katibu mkuu Zanzibar na bara.
Lissu amesema katiba ya chama hicho inataka leo awasilishe jina la,“katibu mkuu wa chama na naibu katibu mkuu wa chama, siyo kesho ni leo.
“Sasa leo saa tisa tutawaleteeni baraza kuu jina la katibu mkuu wa chama chetu, pengine atamrithi Katibu Mkuu, John Mnyika.”
Naibu ni Salum Mwalimu (Zanzibar) na Benson Kigaila upande wa bara. Lissu amempongeza Mnyika kwa kazi kubwa ya kusimamia uchaguzi huo.
Aidha, amesema kilichotokea katika chama hicho (uchaguzi) ni jambo la historia katika siasa za chama hicho na nchi kwa jumla.
Baadaye akitoa hotuba ya kufunga mkutano mkuu huo, Lissu amesema uchaguzi huo umeacha maumivu makubwa: “Lakini hatutalipiza kisasi mimi si mtu wa visasi. Tutawaponya wale wote walioumizwa
na uchaguzi huu ambao tunasema ni wa kihistoria. Tuliingiza taratibu ambazo si za kikatiba, hivyo kama tunataka kuwa salama tutarudi kuwaambia wanachama wetu kwamba hili halitajirudia.”
Katika hotuba hiyo, Lissu amesema moja ya kazi watakayoanza nayo kwa sasa ni kuangazia rufaa zilizokatwa na watia nia wa ujumbe wa kamati kuu ambao kamati kuu iliwaengua kwa sababu mbalimbali.
“Tutaanza na maumivu ya chinja chinja ya wagombea, tutasikiliza rufaa zao kama zina hoja tutawarudisha. Kila mwenye haki ya kugombea uongozi ni lazima apate nafasi hiyo. Lazima tuhakikishe watu wote wanatendewa haki, hatuwezi kudai haki kwa CCM wakati sisi wenyewe ndani hatutendeani haki,” amesema.
Huku akishangiliwa, Lissu amesema: “Kila mwanamke katika chama hiki anayetaka kuwa diwani au mbunge wa kuchaguliwa au viti maalumu ni lazima wapate haki sawa.
“Namna bora ya kufanya hilo, tutaweka ukomo wa viti maalumu hata ikitulazimu kufanya mabadiliko ya katiba na kanuni. Tutaweka pia ukomo wa uongozi wa chama, mimi sitaki kuja kuhutubiwa kwamba nimekaa kwenye uongozi kwa muda mrefu hili litaanza na mimi,” amesema.
Aidha, Lissu katika hotuba yake amesema kwenye uongozi wake hatokuwa na ndimi mbili na kwamba endapo sheria za uchaguzi hazitabadilishwa basi hakuna kufanyika uchaguzi.
Jambo jingine ambalo utawala wake utalifanya ni kurejesha madaraka ngazi ya chini kutoka makao makuu ikiwamo fedha zinazopatikana kuzishusha huko ili kuleta ufanisi na kama hazitokuwapo basi wataelezwa.
Awali, Makamu Mwenyekiti mpya wa Chadema Bara, John Heche amesema majukumu waliyopata ni makubwa hawana budi kuungwa mkono katika kuendeleza mapambano ya chama hicho.
Aidha, amemshukuru Mbowe kwa kujenga uwazi ambao umeonekana kwenye uchaguzi huo.
“Mbowe ameweka standards ambazo hazijawahi kuonekana kwenye chama kingine, Chadema ni chama pekee ambacho watu wake wanaweza kubadilishana madaraka kwa njia za kidemokrasia,” amesema.
“Chadema ni chama, tutakilinda na tunawahidi kukiendeleza, hakuna kulala hadi kieleweke,” amesema.
Heche amempongeza Mnyika kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kusimamia uchaguzi huo pamoja na sekretarieti yake.
“Nimshukuru sana ndugu yangu John Mnyika, ni mtu mwadilifu na msafi sana, nilivyomfahamu tangu siku ya kwanza hadi sasa hajawahi kubadilika. Fikiria kwa presha ile amefanya kazi na mwenyekiti (Mbowe) kwa miaka yote hiyo lakini amesimamia uchaguzi ukiwa amenyooka. Hakutaka kuona aibu na kupindisha mambo,” amesema.
Katika nafasi ya mwenyekiti wa Chadema Taifa, wapigakura waliojisajili walikuwa 1,014 kura zilizopigiwa ni 999, halali zikiwa 996 na tatu zimeharibika.
“Odero Odero kapata kura moja sawa na asilimia 0.1, Freeman Mbowe amepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 huku Lissu akipata kura 513 sawa na asilimia 51.5,” amesema Profesa Raymond Mushi mwenyekiti wa uchaguzi.
Nafasi ya Makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar ameshinda Said Mzee Said ambaye amepata kura 625 sawa na asilimia 89 ya kura 706 huku halali zikiwa 700 na sita zimeharibika.
Katika upande wa Makamu mwenyekiti bara idadi ya wapigakura ni 1, 014 zilizopigwa ni 1005, halali zikiwa 998 na saba zimeharibika.
Matharo Gegul alipata kura 49 asilimia 5, Ezekia Wenje (kura 372, sawa asilimia 37) na John Heche kura 577 sawa na asilimia 57. Hivyo ,Makamu mwenyekiti wa Chadema bara ameshinda Heche.
Uchaguzi huo umesimamiwa na wazee wanane akiwamo Profesa Mushi na Katibu akiwa Dk Azaveli Lwaitama. Wengine ni Ruth Mollel, Ahmed Rashid, Alfred Kinyondo na Azumuli Kasupa.