Pacome afichua kinachoendelea Yanga, atoa ahadi

WIKIENDI iliyopita Yanga ilitoka 0-0 na MC Alger, matokeo hayo yaliifanya kushindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikimaliza nafasi ya tatu Kundi A.

Kushindwa kufuzu robo fainali, kumemfanya kiungo fundi wa timu hiyo, Pacome Zouzoua kutoa kauli ya tumaini jipya.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, waliuanza msimu huu kwa kuivua Simba taji la Ngao ya Jamii.

Baada ya kubeba Ngao ya Jamii, huku Yanga ikishindwa kufikia malengo ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Pacome amesema hawatakubali tena kuona wanawaumiza mashabiki wao hivyo wameamua kurudi kivingine uwanja wa mapambano.

Pacome alisema mpaka sasa hata wao hawaamini kama timu yao imekosa kutinga robo fainali lakini sasa wanajipanga kutetea mataji yao ya ndani.

“Kuna wakati unaona ni kama ndoto kukosa kucheza robo fainali, kuna wakati unapata matokeo ambayo yanashtua, hii imewaumiza sana mashabiki wetu na hata sisi wachezaji,” alisema Pacome na kuongeza.

“Haitakuwa nzuri kama tutawaumiza na kukosa makombe ya ndani ambayo tunayashikilia, tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunatetea makombe yetu yote.”

Nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Dickson Job alisema watakuwa na kazi nzito ya kuhakikisha kila mchezo ulio mbele yao unakuwa na hesabu zake ili kufikia malengo.

“Ujue ligi ni ngumu lakini tuna kikosi cha kuhakikisha tunafanya vizuri, kitu kitakachotusaidia ni kwamba tunataka kila mchezo uwe kama fainali kwetu mpaka tufanikiwe,” alisema Job.

Wikiendi hii Yanga itaanza safari ya kutetea taji la Kombe la FA itakapoikaribisha Copco kutoka Mwanza, mchezo wa hatua ya 64 Bora utakaocheza Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Related Posts