Tshabalala, Kapombe wala kiapo Simba

NAHODHA wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema kitendo cha kuongoza Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufikisha pointi 13, inabaki kuwa mtihani mkubwa kwao ambao wanapaswa kupambana kukabiliana nao hatua zinazofuatia.

Simba kwa kumaliza kinara wa kundi hilo, imefuzu robo fainali ikiwa na faida ya kuanzia ugenini hatua inayofuata ambayo Tshabalala anaamini lazima wafanye kweli ili kuvunja rekodi mbovu waliyonayo.

Beki huyo wa kushoto aliyecheza mechi zote sita za hatua ya makundi, alisema wanatambua wana kazi ngumu ya kufanya ili kuishi katika uhalisia wa malengo yao katika michuano ya CAF ambayo mara tano zilizopita walipocheza robo fainali tangu msimu wa 2018-2019 wameshindwa kwenda nusu fainali.

“Kama wachezaji tunatamani kuandika rekodi ambazo zitaleta heshima kwa klabu yetu, tumeanza na kutinga robo fainali tukishika namba moja katika kundi letu, sasa tunasaka rekodi ya kutinga nusu fainali, kisha tutaendelea na mengine,” alisema na kuongeza.

“Kwa levo ilipofikia Simba hivi sasa ni kubwa Afrika, hata timu zinazopangwa na sisi nazo zinaumiza vichwa namna ya kutukabili kama ilivyo kwetu tunavyoumiza vichwa jinsi ya kukabiliana nao.

“Timu zote zilizotinga hatua ya robo fainali siyo za kuzichukulia poa, zina uwezo lakini kama wachezaji tuna matamanio yetu ambayo tunayapambania ni kutinga nusu fainali kisha kucheza fainali yenyewe.”

Wakati Tshabalala akiyasema hayo, naye beki wa kulia wa kikosi hicho, Shomari Kapombe alisema anajitunza kuhakikisha timu hiyo inafaidi huduma yake kila anapokuwepo uwanjani na anataka kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wanaochezea klabu hiyo.

“Nina uzoefu na michuano hiyo ya kimataifa kwa muda ambao nimeichezea Simba, jambo la msingi najitunza ndio maana napewa nafasi ya kucheza na makocha tofauti, huwa nawaambia vijana endapo kama wataweka umakini katika kazi zao watafika mbali na wataufurahia mpira wa miguu,” alisema Kapombe huku akisisitiza msimu huu wanataka kufika mbali zaidi.

Related Posts