MSHAMBULIAJI Danny Lyanga amesema mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utamjengea heshima kwa kuisaidia Mashujaa aliyojiunga nayo dirisha dogo akitokea JKT Tanzania ambako hakuwa na nafasi kikosi cha kwanza.
Danny ambaye ni mchezaji mzoefu kutokana na kucheza timu mbalimbali zikiwamo Geita Gold, Azam FC, Simba, Fanja ya Oman, Tanzania Prisons na sasa Mashujaa alisema mzunguko wa kwanza kwake haukuanza vizuri na zilikuwa nyakati ngumu ambazo hajawahi kuzipitia tangu aanze kucheza soka.
“Sikuwa majeruhi, ila kocha anakuwa na uamuzi wake wa nani amtumie kulingana na anachotaka katika mechi husika. Nilicheza mechi kama siyo mbili ni tatu tena kwa kupewa dakika chache, bora kama ningekuwa naumwa au majeruhi,” alisema.
“Kwa mara ya kwanza nimepitia nyakati ngumu tangu nianze kucheza soka ndio maana naona faraja yangu pekee kwa sasa ni kwenda kupambana sana Mashujaa ili kurejesha heshima yangu ambayo ilipotea katika mzunguko wa kwanza.”
Alisema anatambua ligi ni ngumu na atakumbana na ushindani wa namba, lakini anaamini mchezaji anapochukuliwa dirisha dogo timu inaongeza nguvu.
“Sitaki kuwaangusha japokuwa nilikuwa sichezi, lakini nilikuwa nafanya sana mazoezi kuanzia ya timu na binafsi, hivyo nipo fiti na tayari kwa kazi na kile nitakachoelekezwa na kocha,” alisema.