Geita. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesajili miradi 901 ya uwekezaji ya Dola 9.3 bilioni za Marekani (Sh23.01 trilioni), kwa mwaka 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 41.6 ya miradi iliyosajiliwa mwaka 2022.
Mwenyekiti wa bodi ya kituo hicho, Dk Binilith Mahenge amesema hayo leo Jumatano Januari 22, 2025 alipotembelea mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Mwamba uliopo Nyarugusu wilayani Geita.
Mgodi huo unamilikiwa na wazawa kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Dk Mahenge amesema kuongezeka kwa miradi hiyo kumetokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji kunakofanywa na Serikali kwa kushirikiana na TIC.
Amesema kwa Mkoa wa Geita, mwaka 2024 walisajili miradi 18 ya Dola 969 za Marekani (Sh2.4 bilioni) na mwaka huu wamelenga kusajili miradi 50.
“Kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji pamoja na sheria mpya ya mwaka 2022 iliyoondoa vikwazo vya uwekezaji, imekuwa kichocheo kikubwa cha watu kusajili biashara zao,”amesema Dk Mahenge.
Amewataka Watanzania kutambua TIC ni yao, hivyo wasajili miradi ili wanufaike na fursa zilizopo ikiwamo za kibiashara, uwekezaji, kilimo, uvuvi na kwa mwaka 2025, wamelenga kusajili miradi 1,500.
Akizungumzia Mgodi wa Mwamba, Dk Mahenge amesema uwekezaji uliofanywa eneo hilo hususan uwepo wa maabara ya kuchakata na kuchenjua dhahabu, utawasaidia wachimbaji wadogo kupata huduma karibu badala ya kubeba sampuli kutoka Nyarugusu hadi Mjini Geita kutafuta huduma.
Akizungumza katika ziara hiyo, Edward Cosnew mwekezaji wa nje aliyewekeza katika mgodi huo, amesema uwekezaji wa kiwanda cha kuchakata na kuchenjua dhahabu walioufanya ni wa Sh8.5 bilioni.
Amesema mazingira rafiki ya uwekezaji yamekuwa chachu kwao kuwekeza nchini na ukarimu wa wenyeji wa eneo hilo, umewafanya waendelee kutamani kuwekeza zaidi ili kuinua uchumi wa Geita.
Meneja wa mgodi huo, Calvin Deogratius amesema mradi huo umejengwa kwa miezi sita na sasa wapo kwenye majaribio ya mitambo.
“Hatujapata changamoto yoyote hata mizigo yetu ilivyokuwa bandarini ilitoka kwa wakati na tumesamehewa kodi, kwa kweli mazingira rafiki ya uwekezaji yanawafanya hata hawa wenzetu kutoka nje kuona Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza,” amesema Deogratius.
Amesema mpaka sasa Watanzania 75 wamepata ajira za moja kwa moja na kila siku hutoa kazi kwa vibarua zaidi ya 20 kwenye mgodi huo.
Kaimu katibu Tawala Mkoa wa Geita, Charles Chacha amesema Geita inazalisha asilimia 70 ya dhahabu inayopatikana nchini na kuwataka wamiliki wa mgodi huo pamoja na wachimbaji wengine, kuzingatia sheria ikiwamo ya kuiuzia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) asilimia 20 ya dhahabu wanayozalisha.