Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho katika uchaguzi uliofanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano, Januari 22, 2025 ameshinda.
Lissu amemng’oa madarakani Freeman Mbowe, aliyekiongoza chama hicho kwa miongo miwili.
Mbowe amekuwa wa kwanza kukiri kushindwa na kumpongeza Lissu kupitia mtandao wa X.
Tundu Lissu, alizaliwa Januari 20, 1968, katika Kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi, Mkoa wa Singida.
Ni mwanasiasa mashuhuri na wakili wa haki za binadamu wa Tanzania.
Akiwa mwanachama wa Chadema, Lissu amejipambanua kwa ujasiri wake wa kukosoa maovu na kupigania haki za kijamii, hata pale ambako usalama wake ulikuwa hatarini.
Alizaliwa katika familia ya wakulima na alikulia katika mazingira ya kawaida kijijini Mahambe.
Lissu alianza safari yake ya kielimu katika shule ya msingi ya eneo hilo kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Ilboru, iliyoko Arusha na alihitimu mwaka 1983.
Baada ya kufaulu vizuri, Lissu alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akichukua Shahada ya Sheria.
Wakati akiwa mwanafunzi, alionyesha mapenzi makubwa kwa haki za binadamu na masuala ya kijamii, ambayo baadaye yalimfungulia njia ya kuwa wakili na mwanaharakati wa haki.
Utaalamu wa sheria na harakati za haki
Baada ya kuhitimu chuo kikuu, Lissu alianza kazi kama wakili wa mazingira na haki za binadamu, akifanya kazi na mashirika kama Lawyers Environmental Action Team (LEAT) na World Resources Institute (WRI).
Wakati akiwa WRI kati ya mwaka 1999 na 2002, Lissu alishirikiana na wenzake kama Peter Veit kushughulikia haki za ardhi za jamii katika maeneo ya migodi ya dhahabu nchini Tanzania.
Alipigania haki za ardhi za jamii zilizokuwa zikihamishwa kwa nguvu kutoka maeneo ya madini na hifadhi za Taifa.
Pia, alihusika katika kufichua ufisadi mkubwa serikalini, akitumia taaluma yake ya sheria kuandaa nyaraka kama vile “List of Shame,” iliyoanika viongozi wa juu waliotuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali za umma.
Mbunge wa Singida Mashariki
Mwaka 2010, Tundu Lissu alijiunga rasmi na siasa kwa kuchaguliwa kuwa mbunge wa Singida Mashariki kupitia tiketi ya Chadema.
Katika kipindi chake bungeni, Lissu alionekana kuwa mbunge mwenye sauti ya kipekee, akitetea masilahi ya wananchi wake kwa bidii. Mwaka 2015, alichaguliwa tena kwa awamu ya pili na aliendelea kukosoa vikali sera za Serikali na kuibua masuala mazito ya kiutawala.
Katika kipindi hiki, Lissu alikamatwa mara kadhaa kwa tuhuma za uchochezi na kumtukana Rais wa wakati huo, John Magufuli.
Hata hivyo, alisisitiza hakukusudia chochote isipokuwa kuleta uwazi na uwajibikaji serikalini.
Jaribio la mauaji la 2017
Alasiri ya Septemba 7, 2017, historia ilichukua mkondo wa kusikitisha katika maisha ya Lissu.
Wakati wa mapumziko ya vikao vya Bunge jijini Dodoma, Lissu alipigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana wakiwa kwenye eneo la makazi ya viongozi Area D jijini Dodoma.
Alipata matibabu Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya hadi Januari 2018 alipohakishiwa nchini Ubeligiji kwa matibabu zaidi.
Tukio hilo ambalo Chadema lilidai kuwa la kisiasa, lilionekana kama tishio kwa demokrasia nchini Tanzania.
Hakuna mtu aliyewahi kutiwa hatiani kwa shambulio hili, jambo ambalo limeendelea kuzua maswali kuhusu mfumo wa haki na uwajibikaji wa vyombo vya dola nchini Tanzania.
Maisha ya uhamishoni na kurudi Tanzania
Kutokana na hofu ya kiusalama, Lissu alikaa Ubelgiji kwa zaidi ya miaka mitatu.
Hata hivyo, Julai 2020, alirudi Tanzania kuwania urais katika uchaguzi mkuu kupitia tiketi ya Chadema.
Aligombea dhidi ya Rais Magufuli, ingawa uchaguzi huo uligubikwa na madai ya ukiukwaji wa demokrasia.
Januari 2023, Lissu alitangaza kurejea tena Tanzania baada ya miaka mitano ya kuishi uhamishoni.
Tangu kurudi kwake, licha ya kukamatwa mara kadhaa, Lissu ameendelea kupigania uwajibikaji wa kisiasa na mabadiliko ya kidemokrasia.
Desemba 2024 alitangaza nia yake ya kugombea kiti cha mwenyekiti wa chama hicho na ameshinda uchaguzi huo.
Lissu ni baba wa watoto wawili pacha na mke mmoja Alicia Magabe ambaye naye kitaaluma ni wakili.