Dk Nchimbi alivyoruka viunzi vya siasa

Usione vyaelea, jua vimeundwa. Ni msemo unaoakisi mikiki mikiki ya siasa aliyopitia Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.

Januari 19, 2025 Dk Nchimbi alipendekezwa kuwa mgombea mwenza wa urais wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan, mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kumwomba Rais Samia apumzike, ombi ambalo lilikubaliwa. Uamuzi huo umepokelewa kwa mitizamo tofauti na wadau, wakiona Dk Nchimbi, anayesifika kwa siasa za kimkakati ni turufu kwa CCM.

Kwa hatua hiyo, Rais Samia atakuwa mgombea urais wa CCM akisindikizwa na Dk Nchimbi katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu. Kuteuliwa kwa Dk Nchimbi kumeendelea kung’arisha nyota yake kisiasa ya kutabiri mema miaka ijayo.

Baada ya Dk Nchimbi kuingia kwenye siasa hapo ndipo mikiki mikiki ikaanza. Alianza safari ya kisiasa akiwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka 1997 na baadaye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mwaka 1998.

Mwaka 2003, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda.

Kada wa CCM, Frank Uhahula aliyegombea naye uenyekiti wa UVCCM mwaka 1998 anasimulia jinsi uchaguzi huo ulivyokuwa mgumu.

“Huo uchaguzi wa 1998 tuligombea wote, ulikuwa mgumu kidogo, hakupatikana mshindi awamu ya kwanza, ikabidi urudiwe na yeye ndiyo akashinda,” anasema.

Licha ya upinzani walioonyeshana, Uhahula anasema Dk Nchimbi alimpendekeza kwenye Baraza la vijana kuwa Katibu wa hamasa na akashika nafasi hiyo akiwa pia mjumbe wa kamati ya utekelezaji.

Kumekuwa na maelezo kuwa ushindani wa Dk Nchimbi na Uhahula uliendelea wakiwa pia UVCCM na ndipo mwaka 2003 wote waliteuliwa na Hayati Rais Benjamin Mkapa kuwa wakuu wa wilaya, Dk Nchimbi akipelekwa Wilayam ya Bunda (Mara) na Uhahula Wilaya ya Chunya.

Hata hivyo, Uhahula amekanusha kuwepo kwa mvutano kati yake na Dk Nchimbi.

“Hayo ni maneno tu, hakukuwa na mvutano. Umoja wa Vijana ndio tanuru la kuoka makada. Mimi kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya sio jambo la ajabu, nimeshakuwa mtu mzima, nimepikwa Umoja wa Vijana na yeye na ili kukuthibitishia, hata wenyeviti waliopita walishakuwa wakuu wa wilaya,” anasema.

Ameongeza: “Kwanza kitendo hiki kwamba tuligombea pamoja, ingekuwa ni mtu wa visasi na uadui, yeye asingenipendekeza kuwa katibu wa hamasa ambayo ilikuwa ni nafasi kubwa UVCCM.”

Uhahula kwa sasa ni mtumishi wa CCM makao makuu na ameendelea kufanya kazi kama msaidizi wa Dk Nchimbi.

Kama ilivyokuwa kawaida, chaguzi za UVCCM zilikuwa na mvutano mkali na ndivyo ilivyokuwa mwaka 2008, ambapo Dk Nchimbi alipata upinzani mkali wa Nape Nnauye. Katika nafasi hiyo aligombea pia Jane Mihanji.

Katika uchaguzi huo, Nape aliibua tuhuma kwa baadhi ya viongozi wa CCM na UVCCM kuwa wamehusika kuingia mkataba ambao hauna maslahi kwa chama.

Hata hivyo, Nchimbi alijibu tuhuma hizo kuwa mkataba huo ulipitishwa kwenye vikao halali na kwamba una maslahi kwa jumuiya hiyo.

Nape alipoulizwa kwa simu kuhusu ushindani huo, hakutaka kuzungumzia.

Mwaka 2005 aligombea ubunge Songea na kushindwa. Baada ya hapo aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri katika wizara mbalimbali, ikiwemo Habari, Utamaduni na Michezo (2006), Kazi, Ajira na Vijana (2006–2008), na Ulinzi na Kujenga Taifa (2008–2010).

Mwaka 2010, alipanda na kuwa Waziri kamili, akihudumu katika Wizara ya Habari na baadaye Wizara ya Mambo ya Ndani hadi Desemba 2013.

Utetezi kwa Lowassa ulivyomponza

Julai 2015 wakati wa uteuzi wa mgombea urais wa CCM, Dk Nchimbi alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliokuwa wakimuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Lowassa.

Miongoni mwa wagombea 17 waliojitokeza, kamati kuu ilikata majina, likiwemo la Lowassa na kuwabakiza Bernard Membe, January Makamba, Dk Asha-Rose Migiro, Dk John Magufuli na Amina Salum Ali.

Baada ya hapo yalikatwa tena majina ya Bernard Membe na January Makamba na hatimaye John Magufuli akapitishwa kuwa mgombea.

Hatua hiyo iliibua hisia kali, hasa kwa wafuasi wa Lowassa na ndipo baadhi ya wajumbe wa kamatiu kuu, akiwamo Dk Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa walizungumza na waandishi wa habari na kupinga kukatwa kwa jina la Lowassa.

Desemba 3, 2016, Dk Nchimbi aliteuliwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil.

Lakini kama wanavyosema, “La kuvunda halina ubani,” Machi 2017 Halmashauri Kuu ya CCM iliibua mashitaka ya Dk Nchimbi, Kimbisa na Sophia wakituhumiwa kukisaliti chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Chama hicho kilimfutia uanachama Sophia Simba na kuwapa onyo kali Dk Nchimbi na Kimbisa.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya kukamilika kwa vikao vya Kamati za Maadili na Kamati ya Kuu ya chama hicho jijini Dodoma, na kisha uamuzi kutangazwa katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa, chini ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais John Magufuli.

Baada ya Rais Samia kuingia madarakani, alimhamisha Dk Nchimbi kutoka Brazil kwenda nchini Misri.

Januari 15, 2024, Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kilichofanyika Zanzibar, kuchukua nafasi ya Daniel Chongolo, aliyejiuzulu Novemba 29, 2023.

Dk Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971, mkoani Mbeya. Atafikisha miaka 54 Desemba mwaka huu.

Elimu yake ya msingi aliipata jijini Dar es Salaam, katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 na 1986.

Dk Nchimbi aliendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Uru (1987–1989) kwa kidato cha kwanza hadi cha tatu, kisha akahamia Shule ya Sekondari Sangu, ambako alihitimu kidato cha nne (1989–1990).

 Kidato cha tano na sita alisoma katika Shule ya Sekondari Forest Hill, Mbeya, kati ya mwaka 1991 na 1993.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alijiunga na kilichokuwa Chuo cha IDM Mzumbe, Morogoro, ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (1994–1997).

 Dk Nchimbi amemuoa Jane Nchimbi na wamejaaliwa watoto watatu.

Related Posts