Moshi. Baadhi ya makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kilimanjaro, wamezungumzia kupatikana kwa safu ya juu ya viongozi wa chama hicho wakisema wanaona mwelekeo mpya.
Hiyo ni baada ya Freeman Mbowe aliyehudumu kama mwenyekiti wa chama hicho kwa zaidi ya miaka 20, kuangushwa na aliyekuwa makamu mwenyekiti wake, Tundu Lissu katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali baina ya wawili hao.
Mbali ya Mbowe kuwa mwenyekiti wa Chadema kwa kipindi hicho, lakini amewahi kuwa mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro kwa vipindi vitatu na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Katika uchaguzi huo Lissu ameshinda kwa kupata kura 513 sawa na asilimia 51.5 dhidi ya Mbowe aliyepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 na Odero Charles Odero akipata kura moja sawa na asilimia 0.1.
Nafasi ya Makamu mwenyekiti bara imechukuliwa na John Heche aliyepata kura 557 kati ya kura 1,005 zilizopigwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Moshi, makada hao wamesema ushindi wa kiongozi huyo utaongeza chachu ya mabadiliko na kuchochea ukuaji wa maendeleo katika jamii.
Devotha Kessy amesema Lissu amekuwa mtetezi wa wanyonge, hivyo kushinda kwake kutawezesha chama hicho kusonga mbele na kuleta mabadiliko katika Taifa.
“Nimefurahi sana kwa ushindi wake, yaani Lissu kushinda nimefurahi mno kwa sababu ni mtetezi wetu na ana malengo ya kutukomboa katika hali tuliyo nayo na atufikishe tunakotaka kufika, tunapenda ufanisi wake,” amesema Kessy.
Ahmed Siwa, mkazi wa Manispaa ya Moshi amesena “Lissu kuchukua jukumu la kuiongoza Chadema kama mwenyekiti, nimeona ni nguvu kubwa sana ya siasa ndani ya chama kwani kama makamu mwenyekiti anaweza kugombea na mwenyekiti na akashinda ni siasa iliyokomaa kabisa na tunategenea makubwa kutoka Chadema.”
Kwa upande wake Rajabu Juma mkazi wa Miembeni amesema ushindi wa Lissu umeonyesha ni namna gani demokrasia imeendelea kukua na kuimarika ndani ya chama hicho.
“Na hii imeonyesha hakuna hatima ya mwenye cheo katika demokrasia, mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi pindi wanachama wanapomtaka mtu wao au wanapoona mtu fulani anafaa katika nafasi ambayo wanaifanyia maamuzi katika uchaguzi.
“Tunashauri viongozi watambue kuwa uongozi ni dhamana na wanawajibika kutimiza yale ambayo wananchi wanayataka ili mwisho wa siku kurudisha imani kwa wale waliowapa dhamana,”amesema Juma.
Naye Shabani Shame amesema: “Mbowe ameonyesha uzalendo kumpongeza Lissu kwa ushindi, na sisi kama wananchi tumefurahia ushindi kwani tulihitaji mabadiliko ya vitendo.”