Unguja. Wakati ugonjwa wa kichaa cha mbwa ukitajwa na wataalamu kutokuwa na dawa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa bure na kuwataka wamiliki wa wanyama hao kujitokeza kuwachanja ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kupitia Idara ya Maendeleo ya Mifugo, imeeleza kuwa itaendelea kutoa chanjo ya maradhi ya kichaa cha mbwa ili kuikinga jamii na madhara ya maradhi hayo.
Akizungumza wakati wa kuzindua mpango huo leo Jumanne, Januari 21, 2025, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mifugo Zanzibar, Asha Zahran Mohammed, amesema hayo huko Ndijani Mseweni wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji chanjo ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya maradhi yanayowakabili mbwa na wanyama wengine wanaofugwa.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina lengo la kutunza jamii yao ili kunusuru maradhi hayo yasiwapate binadamu na ndio maana chanjo hiyo hutolewa bure kwa wanyama hao,” amesema.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kila mfugaji anapaswa kuona umuhimu wa kuchanja mbwa na wanyama wengine kupitia kazi hiyo, kwani kufanya hivyo kutasaidia kuepuka kuhatarisha maisha ya viumbe wengine pamoja na binadamu.
Asha amesema wizara kupitia idara yake imejipanga vema ili kutokomeza maradhi hayo na kuhakikisha mbwa wote wanachanjwa kila mwaka kupitia utaratibu huo, na kwa wafugaji watakaokosa chanjo hiyo wanatakiwa kufika katika kituo cha mifugo ili wanyama wao wapatiwe chanjo hiyo.
Naye Daktari Mkuu wa Mifugo, Ali Mohammed Zahran, amesema ugonjwa huo hauna dawa bali unaweza kuzuiliwa kwa kutumia chanjo, kwani maradhi hayo yanapompata binadamu huwa hayana tiba mahususi badala yake yanaweza kusabisha kifo.
“Kutokana na hilo ndio maana tunahakikisha tunatoa taarifa kwa wafugaji wa kila wilaya na kuwahimiza wafugaji wa mbwa kuwa makini hasa katika suala la chanjo ili mbwa wao waweze kuendelea kuishi vizuri na afya,” ameeleza Dk Zahran.
Amewashauri wafugaji wa wanyama hao kutopuuza wito unaotolewa na mashea kwenye maeneo yao, kwani hili linaweza kuhatarisha maisha.
Awali, Sheha wa Ndijani Mseweni, Masoud Said Abdallah, amesema wamepokea jambo hilo kwa moyo mmoja na kuwashukuru wataalamu wa mifugo kufika katika shehia yao kwani wafugaji wengi waliopo katika eneo hilo wamejitokeza kuchanja mbwa wao.
Omar Said Othman, mmoja wa wafugaji waliojitokeza kuchanja mbwa wao, ameishukuru Serikali kuwaletea chanjo hiyo na kuwataka wafugaji wenzao kuwashughulikia mbwa wao na kuwafikisha katika maeneo yaliyopangwa kupatiwa chanjo ili kuwanusuru na maradhi yanayohatarisha usalama wao na jamii kwa ujumla.
Pia, ametoa rai kuwakamata mbwa wanaozurura ili nao wapatiwe chanjo hiyo, wasiwaambukize virusi vinavyosababisha maambukizi ya maradhi ya kichaa cha mbwa kwa wengine.
Shughuli hiyo inatarajiwa kufanyika katika wilaya ya Kati Unguja, Kaskazini A, Kaskazini B, Wilaya ya Kusini, Wilaya ya Magharibi A, Wilaya ya Magharibi B, na Wilaya ya Mjini kwa Unguja kabla ya kuhamia Wilaya za Pemba.