Shughuli za binadamu zinavyoharibu Mto Songwe, jitihada za kuunusuru zatajwa

Songwe.  Wahenga waliposema ‘Mchuma janga hula na wakwao’ haukuwa msemo ombwe, hii inajidhihirisha kutokana na zaidi ya watu milioni 1.34 wanaotegemea mto huo wako hatarini kuathirika na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na shughuli  za binadamu zinazofanyika pembezoni.

Mkazi wa Kijiji cha Magamba akichota maji pembezoni mwa Mto Songwe. Picha na Pelagia Daniel

Mto huo unaotajwa kuwa tegemeo kwa mahitaji ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya na mkoa jirani wa Songwe kama vile maji ya kunywa, kupikia, kuoga na shughuli zingine za kilimo upo hatarini kukauka.

Mto Songwe wakati wa Kiangazi ambapo kiwango cha maji kimepungua na kuonekana kukauka. Picha na Pelagia Daniel

Madhara yaliyodhahiri ni kupungua na kukauka kwa kina cha maji cha mto, jambo linaloathiri wakazi wa mikoa hiyo.


Shughuli za binadamu zinavyoharibu Mto Songwe, jitihada za kuunusuru zatajwa

 “Tumepoteza baadhi ya mashamba yaliyopo ng’ambo na pembezoni mwa mto, nilikuwa na shamba la miembe ipatayo 20 lakini sasa hivi imebakia mitano” anaeleza Mzee Fransis Mwashuya mkazi wa Kijiji cha Totoe wilayani Songwe.

Mzee huyo anasimulia kuwa miti hiyo ilisombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mmomonyoko wa udogo kwenye kingo za mto zilizotanuka.

Hali hiyo inatajwa ni kutokana na watu kusogeza shughuli zao za kilimo kando ya mito kufuata maji hayo.

Bustani ya mbogamboga zinazolimwa pembezoni mwa Mto Songwe. Picha na Pelagia Daniel

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Galula, Frola Kambaulaya anasema, “Kilimo kimekuwa changamoto awali ulikuwa ukilima heka moja unapata gunia 20 za mahindi tofauti na sasa ambapo unalima heka moja unapata gunia mbili hadi tatu, ardhi imechoka”.

Flora anasema miaka ya karibuni misimu ya mvua imekua haitabiriki. “..Unaweza kulima mvua ikanyesha mara moja tu na inanyesha kidogo, mazao yanaharibika. Hii ni tofauti na ilivyokuwa zamani”.

Tatizo jingine lililotajwa ni kupungua kwa samaki na hivyo kusababbusha bei ya samaki kupaa, wenyeji wakisema kutokana na kupungua kina cha maji cha mto huo.

“…tulikuwa tunapata samaki kwa Sh10,000 kwa sado moja lakini sasa hivi ni Sh20,000 pia tunafuata ziwani na siyo mtoni, tulikuwa tukiuza tunapanga fungu samaki sita kwa Sh2,000 lakini sasa unapata watatu kwa bei hiyo tena ni samaki aina ya magege wadogo,” anasema Joyce Kilolo mkazi wa Kijiji cha Ifuko.

Wazee wasimulia Mto Songwe ulivyobadilika

Akisimulia hali ilivyokuwa ya Mto Songwe katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, Francis Mwashuya (66), mzaliwa wa Kijiji cha Galula wilayani Songwe anasema, “…Nimeukuta Mto Songwe ambapo awali ulikuwa na upana kama mita tatu na kiwango chake cha maji kilikuwa hakikauki.”

Anasema katika kipindi cha nyuma, mto huo ulitumika katika shughuli mbalimbali ikiwamo kufua, kunyweshea mifugo, matumizi ya nyumbani, kujengea, na kupata kitoweo kupitia shughuli ya uvuvi mdogo.

Utunzaji na ulindaji wa mto huo anasema ilikuwa rahisi kwa sababu kulikuwa na idadi ndogo ya watu tofauti na sasa. 

“Zamani, kuna vijiji kama Wanzani, Ndanga Totoe, na Mbuyuni ya Chini ambavyo havikuwa na wakazi wengi, sasa watu wamekuwa wengi, hivyo hadi matumizi ya mto yameongezeka.

Awali, vijiji vilikuwa vichache, lakini sasa hivi kuna vijiji zaidi ya 15 vinavyokaliwa na wakazi wa Wilaya ya Songwe,” aliongeza.

Naye Mwamvi Mwapili (96), mzaliwa wa Kijiji cha Ng’ambo, anasema Mto Songwe ni sehemu ya chanzo bora cha maji kwa matumizi ya binadamu miaka mingi, japokuwa kwa sasa kumekuwa na athari kutokana na matumizi ya binadamu katika chanzo chake. 

“Zamani, mto huo haukuwepo katika kijiji, lakini unasadikika umechepuka na kutengeneza mkondo katika Kijiji cha Ng’ambo na Galula kutokana na mafuriko. Pia, hadithi za zamani zinaeleza kuwa Mto Songwe ulitokana na chemchemu,” anaeleza Mwapili.

Shughuli hatarishi na sheria inavyovunjwa

Licha ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 20 ya 2004 kifungu cha 57 kinabainisha ndani ya mita sitini hakutafanyika shughuli yoyote ya binadamu ya kudumu au ambayo kwa asili yake inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira na, au utunzaji wa bahari au kingo za mto, bwawa, au miambao ya asili ya ziwa, hali ni tofauti kwenye mto huo.

Kumekuwapo na shughuli zinazohatarisha Mto Songwe na mazingira, ikiwemo kilimo cha bustani pembezoni mwa mto, ambapo mashamba mengine yamekaribia kingo za mto. 

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomoni Itunda anasema  uchimbaji wa mchanga na madini unachangia uharibifu wa mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda akizungumza kuhusiana na Mto Songwe alipotembelewa osisini kwake. Picha na Pelagia Daniel

“Wananchi hutumia mchanga kwa ujenzi, huku wengine wakichimba ndani ya mto au makorongo yanayoelekea mtoni. Uchimbaji wa dhahabu pia unasababisha uchafuzi wa mazingira,” anasema. 

Itunda pia anaeleza kuwa ufugaji unaotegemea mto kunyweshea mifugo unasababisha mmomonyoko, uchafuzi wa maji, na hatari ya magonjwa. Ukataji wa majani ya asili kama ‘matete,’ yanayolinda kingo za mto, unafanyika bila kujali athari zake.

Kiasili majani hayo ya asili huota kwa ajili ya kulinda kingo za mto lakini kutokana na ufinyu wa mawazo kwa wananchi wanaona shughuli wanazozifanya ni za kawaida tu.

Naye, Mzee Mwashuya anasema shughuli za uvuvi wa kutumia nyavu zenye matundu madogo ziliharibu mazingira na ingawa Serikali imepiga marufuku, bado uvuvi haramu unaendelea.

Kutokana na shughuli hatarishi zinazofanywa na wakazi wanaozunguka Mto Songwe, kingo za mto zimetanuka kwa upana unaokadiriwa kuwa kilometa moja.

Hali hii inatokana na mmomonyoko kufuatia ukosefu wa uoto wa asili kama ‘matete,’ ambayo yalikuwa yakilinda kingo za mto. 

Sehemu ya Mto Songwe iliyoathirika na mafuriko kufuatia mvua zinazonyesha na kuujaza mto. Picha na Pelagia Daniel

Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Kyela, Godwin Gozbeth, anaeleza kuwa kijiografia, mto unatokea katika Kijiji cha Katumbasongwe wilayani Kyela, mkoani Mbeya, karibu na mpaka wa Tanzania na Malawi. Kwa kuwa eneo hilo lipo ukanda wa chini, mafuriko ya msimu wa masika husababisha mto kujaa na kuhama.

“Huwa tunapata mafuriko kwa sababu kijiografia tupo chini. Mafuriko haya husababisha mto kuhama, na kwa kuwa Mto Songwe ni mpaka kati ya Tanzania na Malawi, wakati mwingine mafuriko huwa upande wa Tanzania na wakati mwingine upande wa Malawi. Hali hii inachangiwa na shughuli za kibinadamu kama kilimo,” anasema Gozbeth.

Mwaka 2019, mvua kubwa ilisababisha Mto Songwe kujaa baada ya kupokea maji kutoka mito midogo kama Mto Momba. Maji hayo, yaliyokuwa yamebeba magogo na miti mikubwa, yaliweza kuezua daraja lililopo Kijiji cha Galula, na kusababisha kukatika kwa mawasiliano katika vijiji 15 vilivyotegemea daraja hilo kwa shughuli za kijamii na kiuchumi. 

Daraja lililoezuliwa wakati wa mafuriko yaliyotokea Mto Songwe katika Kijiji cha Galula wilayani Songwe. Picha na Pelagia Daniel

“Mvua ilinyesha sana siku hiyo nilipokuwa natoka Galula kuelekea Mkwajuni kupeleka maembe sokoni. Nilipofika darajani, hali ilikuwa mbaya; maji yalikuwa yamejaa hadi kufunika daraja. Nilihofia kupita, hivyo nikasubiri maji yapungue. Punde tu, niliona daraja limepasuka na sehemu ya daraja ikabebwa na maji, hivyo mawasiliano yakakatika,” anaeleza mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye hakutaka kutajwa jina.

Uvamizi wa viumbe hatarishi, kupotea kwa samaki

Ongezeko la maji wakati wa masika baadhi ya viumbe kama mamba na viboko kutoka Ziwa Rukwa huhamia mtoni na kuweka makazi ya muda. Viumbe hawa huatarisha usalama wa wanajamii na mifugo yao, na hulazimisha wananchi kuwa waangalifu tofauti na awali walipokuwa wakitumia mto kwa shughuli zao. 

“Wakati wa masika, mamba na viboko huvamia mto na kuweka makazi ya muda. Kipindi hicho huwa tunaogopa kupeleka mifugo mtoni. Kama mwaka juzi, mbuzi watatu wa jirani yangu waliliwa na mamba alipowapeleka mtoni kunywa maji. Hali inakuwa mbaya, tunasubiri maji yapungue ndipo tuendelee na shughuli zetu,” anasema Simoni Isanzu, mkazi wa Kijiji cha Wanzani. 

Shughuli hatarishi kama uvuvi kwenye mazalia ya samaki, mafuriko, na upungufu wa kina cha maji pia zimeathiri upatikanaji wa samaki katika Mto Songwe. Baadhi ya aina ya samaki ambao awali walikuwepo, sasa hawapatikani, na hata samaki wanaopatikana ni wadogo kama Magege. 

“Kutokana na athari hizi, samaki kama Kachaga na Mente hawapatikani tena. Hata samaki waliopo sasa ni wadogo tu,” anaeleza Francis Mwashuya.

Shule, hospitali zilizozama

Mafuriko katika mto yamesababisha mkondo wa maji kuingia katika maeneo ya makazi ya watu, na vijiji vilivyoathirika zaidi ni Totoe, Ndanga, na Mbuyuni Chini.

Zahanati iliyopo katika Kijiji cha Ndanga ambayo huathiriwa na mafuriko yanayotokea katika Mto Songwe. Picha na Pelagia Daniel

Shule na hospitali zimekumbwa na maafa hayo, na wakazi wa baadhi ya vijiji wameamriwa kuhama. Sehemu za shule na hospitali zilizoathiriwa, kama katika Kijiji cha Totoe, sasa zinatumika kwa shughuli za uvuvi. 

Katika Kijiji cha Ndanga, zahanati na shule ya msingi hukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara. Hali hii huwazuia wanafunzi kuhudhuria masomo, na hulazimika kubaki nyumbani hadi maji yapungue.

“Mvua ikinyesha, maji ya Mto Songwe huzunguka shule, na walimu hututangazia tukakae nyumbani hadi hali itulie,” anaeleza mwanafunzi wa Ndanga. 

Pia, mafuriko hayo yamesababisha barabara kupasuka na kutengeneza makorongo, na wakati wa mvua maji ya mto husababisha ugumu wa usafiri. Aidha, miundombinu ya maji imeharibiwa, na mabomba mengine kuchukuliwa na maji, hivyo kuongeza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Sehemu ya barabara katika Kijiji cha Ndanga iliyopasuliwa na Mafuriko yanayotokea katika Mto Songwe. Picha na Pelagia Daniel

Makaburi kufukuliwa na maji

Mafuriko ya wakati wa masika yamesababisha maji kuingia katika makazi ya watu na kuharibu maeneo ya makaburi, hasa katika Kijiji cha Mbuyuni Chini. 

“Mafuriko ya mwaka 2019 yalifukua makaburi na mabaki ya miili kubebwa na maji,” anasema Lukas Mbegeze, mkazi wa Kijiji cha Mbuyuni Chini.

Hatua zinazochukuliwa katika udhibiti

Akifafanua kuhusu uvunjwaji wa sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004, shule, zahanati na madhara mengine Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomoni Itunda, anasema vibao vya tahadhari na katazo vimewekwa kuzuia shughuli zisizoruhusiwa katika maeneo hayo, sambamba na kutenga maeneo ya makazi, malisho, na hifadhi ili kupunguza miingiliano ya binadamu na mifugo inayoweza kuhatarisha mto na kusababisha magonjwa.

Kibango cha tahadhari kilichowekwa katika sehemu ya eneo linalopakana na Mto Songwe. Picha na Pelagia Daniel

Aliongeza kuwa, serikali pia imeanzisha operesheni ya kuwakamata wafugaji wanaokiuka sheria hizo. 

“Mpaka sasa tumewakamata wafugaji wa ng’ombe 15, na kesi zipo mahakamani. Zoezi hili litakuwa endelevu hadi kuhakikisha rasilimali za Wilaya ya Songwe zinalindwa,” anasema Itunda.

Sheria za uchimbaji wa madini pia zinasimamia utunzaji wa mazingira ili kupunguza athari katika Mto Songwe. Itunda anaeleza kuwa mafuriko ya mwaka 2019 yalisababisha uharibifu mkubwa, ikiwemo kuezuliwa kwa daraja na kuharibiwa kwa shule na hospitali katika vijiji vya Totoe na Ndanga.

Serikali imehamisha wakazi wa maeneo hayo na kuwapatia makazi mapya katika Kijiji cha Wanzani. Aidha, ujenzi wa daraja jipya unaogharimu Sh1.5 bilioni unatarajiwa kukamilika Juni 2025, ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii. Kwa sasa, daraja la dharura linatumiwa. 

Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Kyela, Godwin Gozbeth, anaeleza kuwa jitihada za kulinda Mto Songwe ni pamoja na kusimamia sheria ya mita 60, kuruhusu mimea kuota kando ya mto, na kupanda miti. Pia, vifusi vinawekwa kwenye maeneo yenye mianya ili kuzuia maji yasifike makazi ya watu. 

Aidha, Gozbeth ametoa rai kwa Serikali ya Tanzania kushirikiana na Malawi katika utekelezaji wa sheria za mazingira. Anasema shughuli za kilimo pembezoni mwa mto upande wa Malawi zinahatarisha Mto Songwe, na elimu inahitajika ili kupunguza madhara hayo.

Zaidi kuhusu chanzo cha Mto Songwe

Kijiografia, Mto Songwe ni sehemu ya Bonde la Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania. Mto huu unaanzia katika Mkoa wa Mbeya vijini wilayani Kyela kijiji cha Katumbasongwe unapita katika vijiji vinavyokadiriwa kuwa zaidi ya 15 na kumwaga maji katika Ziwa Rukwa.

Mto Songwe unaunda sehemu ya mpaka kati ya Tanzania na Malawi na una urefu wa kilometa 200.

Bonde la Mto Songwe lipo Kusini Magharibi mwa Tanzania na Kaskazini mwa nchi ya Malawi na lina ukubwa wa kilometa za mraba 4,243. Mto huu hutumiwa zaidi ya wakazi 1.34 milioni katika shughuli mbalimbali ikiwamo kijamii na kiuchumi.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts