Safari ya Yanga hadi kubeba ubingwa 2023/2024

YANGA imejihakikishia ubingwa jana baada ya kuichapa Mtibwa Sugar na kujikusanyia taji la 30 kihistoria la Ligi Kuu Bara lakini msimu huu ikiwa na rekodi hizi za kuvutia msimu huu unaoelekea ukingoni.

Ilianza kwa kupoteza Ngao

Yanga iliuanza msimu kwa mshtuko baada ya kupoteza taji la kwanza mapema tu kwenye mechi za ngao ya jamii  ikianza kwa kushinda 2-0 dhidi ya Azam lakini kwenye fainali ikajikuta inalipoteza taji hilo ililolishikilia kwa misimu miwili mfululizo baada ya Simba kushinda kwa mikwaju ya penalti (3-1).

Msimu huu wa ligi ulipoanza Agosti 23,2023 ndani ya mwezi huo Yanga ilicheza mechi mbili za ligi ikishinda kwa kishindo cha mabao 5-0 kila mmoja ikitangulia kuichapa KMC na baadaye JKT Tanzania ikikusanya pointi zake sita za kwanza na mabao 10.

Ndani ya mwezi Septemba ulichangia pointi tatu pekee kwa Yanga kwenye ubingwa huu ilipoichapa Namungo ya Lindi kwa bao 1-0 kwenye mchezo ambao ulikuwa mgumu bingwa mtetezi akijihakikishia ushindi dakika za jioni. hatua ya makundi.

OKTOBA POINTI TISA,KIPIGO

Ndani ya mwezi Oktoba Yanga ikaunza kwa mshtuko ikipoteza mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Ihefu kwa mabao 2-1 kipigo kilichojirudia kama cha msimu uliopita ilipopoteza kwa matokeo kama hayo.

Baada ya kipigo hicho Yanga ikarudi kwenye utulivu na kushinda mechi zake tatu ndani ya mwezi huo ugenini dhidi ya Geita (0-3), ikashinda mechi zingine mbili za nyumbani dhidi yas Azam (3-2) kisha Singida Fountain Gate (2-0) ikijikusanyia pointi tisa.

NOVEMBA POINTI SITA NA MTANI

Bingwa mtetezi aliendelea kuuwasha moto ikishinda michezo miwili ya ugenini ndani ya mwezi Novemba, ikianza kwa kuichapa Simba kwa kishido cha mabao (5-1) kisha Coastal Union (0-1) na kujikusanyia pointi sita lakini utamu kwao ukawa ni ushindi dhidi ya wekundu hao ikilipa kisasi cha kupoteza kama hivyo kwa miaka

Ikifunga mwaka Yanga ndani ya mwezi Desemba ilicheza mechi mbili za ligi dhidi ya Mtibwa Sugar nyumbani (4-1) kisha ile ya ugenini dhidi ya Tabora United kwa bao (1-0) ikifunga mwaka kwa alama sita lakini ikawa imejikusanyia jumla ya pointi 30 ndani ya mwaka 2023.

Ndani ya mwaka 2024 baada ya kupisha Fianali za Kombe la Mapinduzi na hata Fainali za Mataifa Afrika ligi iliendelea mwezi Februari na hapa safari ya Yanga kwenda kutetea taji lao kwa msimu wa tatu mfulilizo iliendelea kibabe ikicheza mechi sita za ligi ilikusanya jumla ya pointi 13 ikishinda mechi tano dhidi ya Dodoma jiji (1-0), Mashujaa (2-1),Tanzania Prisons (2-1) kisha sare ya kwanza  ya msimu ugenini dhidi ya Kagera Sugar (0-0) kisha ikaanza mzunguko wa pili kwa ushindi wea mabao (3-0) dhidi ya KMC.

MACHI POINTI SITA, KIPIGO TENA

Ndani ya Machi Yanga ikawa na mechi tatu za ligi ikishinda mbili dhidi ya Namungo (1-3),Geita (1-0) kisha ikashtuliwa tena pale ambapo Azam ilipolipa kisasi bingwa mtetezi akilala kwa mabao (2-1), ikipoteza mechi ya pili ndani ya msimu.

APRILI POINTI 16, MTANI TENA

Yanga ndani ya mwezi Aprili ikacheza jumla ya mechi sita ikishinda tano dhidi ya Singida Fountain Gate (3-0),Coastal Union (1-0),Kagera Sugar (1-0) lakini utamu mkubwa kwao ukawa ni kuifunga tena Simba kwa mabao (2-1) kisha ikitoa sare ya bila mabao dhidi ya JKT Tanzania ikikusanya jumla ya pointi 16.

Yanga msimu huu kwenye mechi zake 22 za ushindi kabla ya mechi ya jana dhidi ya Mtibwa imeshinda mechi zote 13 za nyumbani na kukusanya pointi 39 ikiwa ndio timu iliyoshinda mechi nyingi ikiwa kwake.

Achana na hilo kubwa zaidi ni kwamba mara ya mwisho Yanga kupoteza nyumbani kwenye ligi ilikuwa Aprili 25,2021 ilipolala nyumbani kwa bao 1-0 la mshambuliaji Prince Dube ambapo baada ya mechi hiyo Yanga imecheza jumla ya michezo 43 nyumbani bila kupoteza.

Yanga imeshinda mechi nane kabla ya mchezo wa jana kwa mechi za ugenini ambapo mechi mbili ilizopoteza za ugenini dhidi ya Azam na Ihefu lakini zile sare za ugenini dhidi ya JKT Tanzania na Kagera zikiwatibulia wakati ikisalia na mechi tatu.

SIMBA, WENZAKE SITA MARA MBILI

Simba na wenzake, Singida FG,Coastal Union,Mashujaa,KMC,Geita na Namungo ndio timu zilipoipa Yanga pointi sita kila moja baada ya kufungwa nje ndani na mabingwa hao kabla ya mechi ya jana dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kiungo mshambuliaji Stephane Aziz KI ndiye mtu hatari kwenye ubingwa wa Yanga msimu huu akiwa na mabao 15 na asisti nane akiibeba Yanga kutoka kwa aliyekuwa mshambuliaji wao Fiston Mayele ambaye alifunga mabao 17 na kuwa mfungaji bora msimu uliopita.

Yanga msimu huu kama unatafuta nani amewabeba basi jibu litakuwa rahisi ni viungo wa timu hiyo ambao wamefunga jumla ya mabao 42 wakiwapiga bao washambuliaji ambapo viungo walioobeba ni Aziz KI (15),Maxi Nzengeli (9),Mudathir (9),Pacome Zouzoua (7),Mahaltese Makudubela (1) na Agustine Okrah (1).

Washambuliaji wao kinara wao ni Joseph Guede ambaye licha ya kuingia dirisha dogo la usajili ndio anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao matano akifuatiwa na Clement Mzize (4), Kennedy Musonda (3) Hafiz Konkon (1) wakati beki pekee aliyefunga kabla ya mchezo wa Mtibwa ni Yao Akouassi (1).

Msimu huu kabla ya kumalizika kama kuna timu imeshinda kwa mabao matano basi Yanga itaongoza ikiwa imezifunga timu nne kwa idadi hiyo ya mabao ambazo ni KMC,JKT Tanzania, Simba na Ihefu

Yanga ndio timu pia iliyoruhusu mabao machache zaidi kwenye ukuta wake ikiruhusu mabao 13 pekee   ikifuatiwa na Coastal Union iliyoruhusu mabao 18 kisha wako Simba nafasi ya tatu iliyoruhusu mabao 20.

Related Posts