Masheha sasa kuhudumia wananchi kidijitali

Unguja. Masheha kisiwani hapa wameanza kutumia mfumo wa kidijitali kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi na kwa haraka. Mfumo huu, unaojulikana kama eDUA, ni lango kuu la utoaji wa huduma za serikali likilenga kupunguza gharama za matumizi ya karatasi, muda na usumbufu wa kupanga foleni kwa wananchi.

Haya yamesemwa leo mjini Unguja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGaz), Said Seif Said, wakati wa mafunzo ya masheha wa Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini na Magharibi.

Said amesema mfumo huo umetengenezwa kwa kushirikiana na kampuni ya Mix by Yas kama sehemu ya jitihada za kuelekea serikali ya kidijitali.

Amesema  mfumo huu utasaidia pia kurahisisha huduma kwa wananchi kupitia teknolojia ya kisasa.

“Hii ni hatua kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za serikali kwa urahisi kupitia sehemu moja. Tumepata mwitikio mkubwa kutoka kwa masheha,” amesema Said huku akibainisha kuwa masheha wote wataunganishwa na mtandao na kupewa vitendea kazi vinavyofaa.

Pia, amesema huduma zinazohusisha idhini ya sheha, zitakuwa rahisi zaidi, huku mfumo huo ukiruhusu kutoa vibali moja kwa moja hata nyakati za usiku kupitia simu za mkononi. “Malipo yatafanyika kidijitali, hakuna karatasi zitakazotumika, hii ni mfumo wa ‘zero paper’ na ‘zero root’,” aliongeza.

Kwa upande wake, Salum Nassor Ahmed, Meneja wa Mix by Yas Zanzibar, akizungumza katika mafunzo hayo, amesema kampuni yake inashirikiana na eGaz kuhakikisha mawasiliano na malipo ya kidijitali yanafanikiwa kwa ufanisi. “Haya ni mapinduzi makubwa ya kidijitali, na tunajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko haya,” amesema.

Naye Hamid Seif Said, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, amebainisha kuwa mfumo huo utapunguza changamoto za kupotea kwa taarifa za karatasi na kuimarisha utendaji kazi wa masheha. “Masheha ni kiungo muhimu cha kwanza katika utoaji wa huduma, na mfumo huu unaleta urahisi mkubwa kuanzia ngazi za chini,” amesema.

Masheha walioshiriki mafunzo hayo wamepongeza mfumo huo, wakisema utarahisisha kazi zao.

Mariam Laban, sheha wa Shehia ya Mpendae, amesema, “Tulikuwa tunategemea maandishi, lakini sasa kupitia mifumo ya mtandao, kazi zitafanyika kwa haraka na kwa ufanisi.”

Hatua zinazofuata ni kutoa mafunzo kwa wananchi ili kufanikisha matumizi bora ya mfumo huu wa kidijitali, hatua inayotarajiwa kubadilisha kabisa jinsi huduma za serikali zinavyotolewa kisiwani Zanzibar.

Related Posts