Vijana kutumia vipaji vyao kujiajiri

Unguja. Vijana wametakiwa kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kujiajiri badala ya kutegemea ajira serikalini. Wito huo umetolewa na Balozi wa Vijana Zanzibar, Mohammed Salim Mohammed, Leo Jumatatu Januari 20, 2025, alipotembelea miradi ya kilimo ya Baraza la Vijana Shehia ya Miwani, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Balozi Mohammed amesisitiza kuwa serikali inatoa msaada mkubwa kwa miradi ya vijana, hivyo ni jukumu lao kuchangamkia fursa hizo. “Vijana wana vipaji vya aina mbalimbali. Wakitumia vipaji hivyo kwa bidii na kuanzisha miradi yao, wataweza kujiajiri na kutengeneza fursa zenye faida kwao,” amesema.

Aidha, amebainisha kuwa Zanzibar ina ardhi nzuri kwa kilimo ambayo vijana wanapaswa kuitumia ipasavyo ili kufanikisha malengo yao.

Balozi huyo pia ametoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kwa juhudi zake za kuimarisha maendeleo ya vijana na kuwaunga mkono katika kujiajiri na kuajiri wengine.

Akizungumza awali, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Shehia ya Miwani, Seif Hassan Seif, amesema vijana 35 wameungana na kuanzisha mradi wa kilimo cha bamia na muhogo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kupunguza utegemezi wa familia.

Hata hivyo, amebainisha changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa kumiliki ardhi na matatizo ya upatikanaji wa maji, hasa wakati wa kiangazi. “Changamoto hizi zinatufanya tuwe na hofu ya kukosa shughuli za kufanya. Hadi sasa tunatumia eneo ambalo si letu, na tunaweza kuondolewa wakati wowote mmiliki anapolihitaji,” amesema Seif.

Kwa upande wake, Zainab Salum Ahmad, mmoja wa wanachama wa baraza hilo, amewahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika kuanzisha miradi ili kujiondoa kwenye utegemezi wa kifamilia, hali ambayo alisema inashusha hadhi yao.

Akizungumzia suala la utegemezi wa vijana kwa familia, Jamila Abdalah Sheikh amesema unachangia mzigo mkubwa kwa wazazi, mdugu na Taifa kwa ujumla.

“Vijana wanaotegemea familia kwa mahitaji yao ya kila siku, kama chakula, malazi, mavazi wanaongeza gharama kwa wazazi,” amesema.

Hata hivyo, amesema kama vijana watazitumia vema fursa zinazowazunguka watauepusha mzigo huo kwa familia na Taifa.

Amesema familia zinazobeba mzigo wa vijana wasiojitegemea mara nyingi hushindwa kuweka akiba au kuwekeza katika rasilimali za baadaye ikiwema ardhi, nyumba, au biashara.

Related Posts