Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emanuel Tutuba amesema kuwa Noti Mpya za
Tanzania zenye Saini ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck
Nchemba (Mb) na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye
mzunguko kuanzia tarehe mosi Februari mwaka huu.
Gavana
Tutuba amesema hayo wakati akimkabidhi Mhe. Dkt. Nchemba, Noti kifani
za shilingi elfu kumi, elfu Tano, Elfu Mbili na Shilingi Elfu moja,
katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, kwa mujibu
wa Sheria na Taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
“Mheshimiwa
Waziri, ninayofuraha kukujulisha kuwa zoezi letu la uchapaji upya wa
Noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika na tayari
tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la
Serikali” alisema Bw. Tutuba.
Gavana
Tutuba alifafanua kuwa Noti hizo zitatumika sambamba na Noti zilizopo
hivi sasa, zinamwonekano wa Noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa
Mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine,
isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania.
“Saini
ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
imebadilishwa na kuwekwa Saini yako Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na
Saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Prof.
Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa Saini ya Gavana wa Benki Kuu wa
sasa, Bw. Emmanuel Tutuba” aliongeza Bw. Tutuba.
Akizungumza
baada ya kupokea sampuli za Noti hizo mpya, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa
Noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka
kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaendeleza
heshima ya wataalam wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo yenye
maslahi mapana kwa nchi yetu” Alisema Dkt. Nchemba.
Mhe.
Dkt. Nchemba aliridhia Noti hizo ziingizwe kwenye mzunguko na kuanza
kutumika kama ilivyopangwa tarehe moja Februari mwaka huu.
Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto), akipokea
Noti Mpya kifani za shilingi elfu kumi, elfu Tano, elfu Mbili na
shilingi elfu moja, kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.
Emmanuel Tutuba, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es
Salaam, Noti ambazo zitaanza kutumika sambamba na Noti zilizopo hivi
sasa, kuanzia tarehe Mosi Februari, 2025.