MBIO za mita 3000 kuruka viunzi na maji (steeplechase) zimekuwa ni mtihani usio na majibu kwa miaka 45 sasa tangu Filbert Bayi azitumie kuipatia Tanzania medali ya fedha katika michuano ya Olimpiki ya Moscow, Urusi mwaka 1980.
Tangu Bayi aishindie Tanzania moja ya medali mbili za pekee za Olimpiki, hakukuwapo na harakati zozote za wanariadha wa Tanzania kutaka kuikaribia wala kuivunja rekodi ya Bayi ya dakika 8, sekunde 12 na nukta 48, ambayo hivi leo inakaribia miaka 45.
“Mita 3000 steeplechase ni mbio ngumu na za hatari kwa sababu unaruka viunzi virefu na maji kwa pamoja. Mimi niliamua kujaribu mbio hizo baada ya kuona umri umezidi kusogea miaka sita baada ya kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 mjini Christchurch, New Zealand mwaka 1974,” Bayi alifafanua sababu iliyomfanya asikimbie tena mbio za mita 1500 na kujaribu mbio ndefu za kuruka viunzi na maji.
Ingawa imepata washiriki wengi miaka ya hivi karibuni, hata rekodi nyingine ya Bayi ya dakika 3 sekunde 32 na nukta 16 bado haijuvunjwa wala kufikiwa kwa miaka 51 sasa.
Haiwashangazi wadau wa riadha kwa rekodi ya mbio za mita 3000 kuruka viunzi kuendelea bila kuvunjwa kwa sababu hakuna mwanariadha anayezitilia maanani, lakini mita 1500 ambazo mwanaridha anazunguka uwanja mara nne, haieleweki ni kwa nini wengi wanashindwa kuifikia au kuvunja rekodi ya Bayi.
“Ni vigumu kuvunjwa kwa sababu kwa Watanzania wa leo kila mbio kwao ni marathon, hakuna kingine zaidi,” alisema mwalimu wa mbio fupi jijini, Iddi Mhunzi.
Rekodi ya pekee ya Bayi iliyofikiwa na kuvunjwa ni ya mita 800 ambayo ilivunjwa na Samuel Mwera mwaka 2005 mjini Rio de Janeiro, Brazil ambapo alitumia dakika 1, sekunde 45 na nukta 28. Bayi aliweka rekodi hiyo mwaka 1974.
Mwera ni mwanariadha wa pekee kushinda medali ya dhahabu katika michezo ya All African Games ya mwaka 2005 katika mita 800 na baadaye mwaka huo huo kushinda medali ya shaba katika michezo ya India na Afrika.
Wanariadha wakongwe nchini Simon Mrashani na Oswald Revelian walikuwa na majibu mazuri ya kwa nini mbio fupi (sprint) na za masafa ya kati hazitiliwi mkazo na wanariadha.
“Mialiko ya kimataifa inayowatambua Watanzania kama mabingwa wa mbio za masafa marefu ndiyo inawafanya Watanzania kutozipenda mbio fupi (sprint) na mbio za masafa ya kati (middle distance races) kuanzia meta 800, 1500 na 3000 kwani mialiko mingi inakuwa ya mbio ndefu na ngumu za kilometa 21 (half marathon) na 42 (full marathon),” alisema Levelian ambaye pia ni mkimbiaji wa mbio za marathoni.
Nani aliyeifanya Tanzania kuwa ni nchi ya marathon wakati dunia inaona kuwa ni meta 3000 steeplechase na meta 5000 pekee ndizo zilizoipa Tanzania medali pekee za Olimpiki mwaka 1980?
Wanariadha wakongwe; Nada Meta na Jumanne Tluway kutoka Mbulu walimtaja Juma Ikangaa kama mwanaridha aliyeionysha dunia kuwa Tanzania ndiyo chimbo la mbio za masafa marefu ikiwamo marathon.
Kauli ya wanariadha hawa wakongwe inaungwa mkono na rekodi ambazo zinambeba Juma Ikangaa na wengine wengi waliofanya vizuri kufuatia mafanikio yake.
Katika michezo mikubwa ya kidunia kama IAAF World Athletics Championship, Michezo ya Jumuiya ya Madola na hata All African Games, Watanzania wametamba katika marathon, nusu marathon na mbio za mita 10,000.
Aliyejuu kwa sasa ni Gabriel Geay ambaye anashikilia rekodi ya marathon ya saa 2, dakika 03 na sekunde 00 aliyoiweka mwaka 2022 huko Valencia, Hispania.
Mabingwa wengine wa mbio za masafa marefu waliopeperusha vyema bendera ya Tanzania ni pamoja na Gidamis Shahanga, Zakaria Barie, Simon Mrashani, Geway Suja na Samson Ramadhan.
Wengine ni Fabian Joseph, Martin Sulle, Christopher Isegwe, Francis Naali, John Yuda Msuri, Emanuel Giniki na Alphonce Simbu.