Josiah: Ishu ya wakongwe ni nje ya uwezo wangu, nakomaa na hawa Prisons

Mbeya. Kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah amesema kuondoka kwa baadhi ya nyota wake ni pengo, lakini usajili mpya utaweza kuziba upungufu na timu kufanya vizuri.

Katika dirisha dogo lililofungwa Januari 15, Prisons imesajili wachezaji sita, huku wakiondoka mastaa wake sita waliokuwa watumishi wa Magereza ambao tayari wamepangiwa majukumu mengine.

Walioondoka ni wakongwe Salum Kimenya, Jumanne Elfadhil, Samson Mbangula, Jeremia Juma, Nurdin Chona na Jamal Masenga, ambao ni waajiriwa wa Jeshi la Magereza.

Wamo pia walioondoka ambao hawakuwa askari, Zabona Hamis, Ally Msengi na Hamis Kasanga aliyepelekwa timu ya vijana ya Magereza Dar es Salaam.

Kwa upande wa walioingia ni Yusuph Athuman, Kelvin Sabato ‘Kiduku’, Rabin Sanga, Hamad Bumage, Adam Adam na Sufian Yusuph kutoka Zanzibar ambao baadhi yao wameshaungana na timu tayari kusubiri Ligi Kuu mzunguko wa pili itakaporejea Februari 6 kuikabili Mashujaa.

Josiah amesema hawezi kubeza mchango wa wakongwe hao ambapo mengine ni mipango ya uongozi akieleza kuwa kwa sasa anakomaa na waliopo kuhakikisha anafikia malengo.

Amesema kwa muda ambao wamekuwa na maandalizi anaridhishwa na mapokeo ya nyota wake akitamba kuwa kwa mwenendo walionao wanaweza kurejea na nguvu mpya mzunguko wa pili.

“Lazima tukubali mchango wa walioondoka, mengine ni nje ya uwezo wangu, ninachopambania ni kutengeneza muunganiko kwa waliopo na bahati nzuri wameonyesha kunielewa na matarajio ni kuanza mzunguko wa pili kwa nguvu mpya.”

“Nimekuwa na mechi za kirafiki kama tatu, lakini ya leo dhidi ya Ken Gold nimeona kila mmoja anapambana kuonyesha uwezo wake na hadi sasa tuko tayari kwa Ligi Kuu,” amesema Josiah.

Straika wa timu hiyo, Yusuph Athuman amesema kuingia kikosini humo na kufunga bao katika mchezo wa kirafiki kwake ni mwanzo mzuri unaoonesha mwanga katika kazi ya soka.

Amesema kutokana na uwezo na uzoefu alionao katika soka la ushindani, anatamani kuona anaifanyia kazi timu hiyo na kuondoka nafasi iliyopo kwa sasa na kuwa sehemu nzuri kwenye msimamo.

“Ni mwanzo mzuri na kazi ya straika ni kufunga mabao, matarajio ni kuona naipambania timu kuhakikisha tunabaki Ligi Kuu kwakuwa hadi sasa hatuko sehemu nzuri,” amesema nyota huyo wa zamani wa Mbao, Biashara United na Yanga.

Related Posts