KITASA wa Fountain Gate, Joram Mgeveke, amekiri pamoja na kukutana na washambuliaji tofauti katika maisha ya soka, lakini ukweli hakuna aliyekuwa hatari kama Fiston Mayele alivyokuwa akicheza Ligi Kuu Bara katika kikosi cha Yanga.
Mgeveke ambaye amecheza dhidi ya washambuliaji wengi na tishio, alisema kuwa Mayele alikuwa na sifa za kipekee zilizomfanya kuwa mchezaji ambaye alijua jinsi ya kuwasumbua mabeki wa timu nyingi nchini.
Akizungumza kuhusu Mayele, ambaye kwa sasa anachezea Pyramids FC ya Misri, Mgeveke alisema: “Nisingeweza kusema kwamba hakuna washambuliaji wazuri kwenye ligi yetu sasa, lakini ni wazi kwamba Mayele alikuwa na kitu cha pekee.
“Alikuwa na kila kitu ambacho mshambuliaji wa kisasa anatakiwa kuwa nacho. Alikuwa na kasi, nguvu, ufanisi wa kumalizia nafasi, na pia akili za kimchezo ambavyo vilimfanya kuwa hatari kwa mabeki. Kila timu ilijua kuwa anapaswa kupewa umakini mkubwa hasa akiwa kwenye eneo la hatari.”
Mayele alifanya historia kubwa katika Ligi ya Tanzania alipojiunga na Yanga, ambapo alifunga mabao 50 katika mechi 54. Katika msimu wake wa mwisho wa 2022/23, alitwaa tuzo ya mfungaji bora wa ligi akiwa na mabao 17, sawa na Saido Ntibazonkiza wa Simba.
Mgeveke alikiri, alikumbana na changamoto kubwa kumzuia Mayele; “Unajua, kumshika Mayele uwanjani ilikuwa ni kazi ngumu sana. Alikuwa na uwezo wa kutetema, yaani alikuwa akiwatesa mabeki kila alipokuwa kwenye mpira. Tulijua kuwa hatuwezi kumzuia kirahisi, hivyo ilikuwa ni lazima kuwa na maandalizi ya ziada ili kumkaba,” Mgeveke alisema kuhusu Mkongomani huyo.