Dar es Salaam. Uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ndicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, umemalizika lakini kinahitaji upatanishi wa kweli kama kinataka kubaki salama na kuingia uchaguzi mkuu wakiwa wamoja.
Haitakuwa mara ya kwanza kwa chama cha siasa hapa Tanzania kuunda kamati ya upatanishi, kwani mwaka 2009, Chama cha Mapinduzi (CCM), kiliwahi kuunda kamati iliyojulikana kama ‘Kamati ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi’.
Kamati hiyo iliundwa mahususi kuwapatanisha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanaotokana na CCM, ambao walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili, wakinyukana na kutuhumiwa kwa mambo mbalimbali.
Katika kamati hiyo ambayo iliendesha shughuli zake kwa faragha ndani ya kumbi za Bunge, na ambayo ilikuwa na sifa zote za kuwa kamati ya ukweli na maridhiano, wabunge walinyukana hasa lakini mwisho wa siku walipatana na kuwa kitu kimoja.
Ni kupitia kamati hiyo, tulisikia tuhuma nzitonzito za baadhi ya wabunge kushutumiana kupokea fedha za watuhumiwa wa ufisadi na wengine wakituhumiana kutokana na mmoja kukosa kuwa mke wa Rais au ‘First Lady”.
Mbunge mmoja wa viti maalumu aliyekuwa na wadhifa pia ndani ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), alimtuhumu mwenzake kuwa ana nongwa kwa sababu tu ya hasira zinazotokana na mumewe kutoteuliwa kuwa mgombea urais.
Hata 4R alizoziasisi Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuapishwa kuwa Rais Machi 2021, baada ya John Magufuli zilikuwa na lengo la kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.
Sitaki kuingia kwa undani mafanikio hayo ya 4R lakini ninasema Chadema leo wakija na utaratibu wa kuunda kamati ya ukweli na upatanishi, watakuwa wanatembea humohumo na lengo ni kutibu majeraha ya uchaguzi wao.
Katika uchaguzi wa Chadema ambao kwa mtu yeyote mwenye akili atakubaliana na mimi kuwa umeacha majeraha makubwa, Tundu Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti kuchukua nafasi ya Freeman Mbowe aliyeongoza takribani miaka 21.
Kura 513 sawa na asilimia 51.5 alizozipata Lissu na 482 au asilimia 48.3 ambazo alizipata Mbowe, ni ushahidi tosha kuwa uchaguzi huo haukuwa lelemama, bali uliokuwa umejaa kila aina ya ushindani wa kweli na wa kidemokrasia.
Upatanishi huo ni muhimu sana kama vile uji ulivyo na umuhimu kwa mgonjwa kwani dunia imeshuhudia minyukano isiyo ya kawaida, kutuhumiana mambo mazito na hata matumizi ya lugha isiyo ya kistaarabu kwa baadhi ya wapambe.
Tulishuhudia kila kiongozi ndani ya chama akiwa na sharubu kama kambale kiasi kwamba kila mmoja aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwashambulia ama Lissu au Mbowe kama njia ya kupata uungwaji mkono katika uchaguzi.
Tulishuhudia wapambe wakitumia mitandao ya kijamii ya X, Instagram, Facebook, WhatsApp, YouTube na vyombo vya Habari kama televisheni na radio kushambuliana na kuwashambulia wagombea hata kwa tuhuma za uongo.
Huo ndio ukweli na ukweli siku zote una sifa moja kuu kwamba hata ukiuchukia au kuukataa, haugeuki kuwa uongo hivyo Chadema kama wanataka kubaki wamoja, hawana budi kutafuta upatanishi tena haraka kabla ya uchaguzi mkuu.
Ninakubalia na Mbowe ambaye katika hotuba ya kuwaaga wajumbe wa mkutano mkuu jana katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, aliwaagiza viongozi wapya waliochaguliwa kuona umuhimu wa kufanya mapatano.
Mbowe amesisitiza sana kuwa uchaguzi wao huo umeacha majeraha makubwa , kauli ambayo iliungwa mkono na Lissu wakati akifunga mkutano huo mkuu akisema wataleta tumaini jipya na kuwarudisha wale waliokata tamaa.
Ni kweli, wapo wanachama, wafuasi, wapambe na hata Watanzania walitamani Mbowe aendelee kuwa kiongozi, na wapo waliotaka Lissu ndio awe kiongozi, sasa hulka ya mwanadamu huwa na kinyongo pale anayemtaka asipokuwa kiongozi.
Hata kama uchaguzi uwe wa huru, haki na uwazi kiasi gani, kwa aina ya kampeni zilizoshuhudiwa zimeacha mpasuko mkubwa na wapo wanatamani kujitoa bila kufahamu uchaguzi una matokeo mawili tu, ama kushinda au kushindwa.
Uchaguzi ukiisha na makundi yanatakiwa kufa na kila kundi litambue sio mtu ameshinda bali chama ndicho kimeshinda na minyukano iliyoonekana haipaswi kukigawa chama hicho, bali uchaguzi huo uwaimarishe zaidi na zaidi.
Ukiwa na wanachama wa aina hiyo hao imani ya chama inakuwa haiko mioyoni mwao, wanamfuata mtu badala ya itikadi, hivyo vikao vya ukweli na upatanishi ni muhimu sana ili Chadema iende uchaguzi mkuu kikiwa na uungwaji mkono.
Lazima ifahamike kuwa hata CCM chenyewe kinahitaji upinzani imara, na hata wananchi wanahitaji upinzani imara ili chama kilichopo madarakani kisijisahau, kwa hiyo ili Chadema iendelee kuwa taasisi imara, ni lazima wawe wamoja.
Uchaguzi wa Chadema umefuatiliwa si tu na Wanachadema na wafuasi wao, hapana, uchaguzi huo umefuatiliwa na mamilioni ya Watanzania na wapenda demokrasia duniani wakiwamo wana CCM. Ni kwa sababu kuna tumaini ndani yao.
Kauli ya Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Tundu Lissu ya kwenda kushughulikia makovu ya chaguzi si huu pekee bali hadi ule wa ngazi za chini, inapaswa kutekelezwa kwa vitendo haraka iwezekavyo hasa ikizingatiwa pasi na kufanya hivyo wanaweza kuingia kwenye uchaguzi mkuu wakiwa vipande viwili. Tume hiyo inapaswa isiwe ya kutiliwa mawaa ili itekeleze wajibu wake ipasavyo.